Maandamano yaliendelea katika mji mkuu wa Kenya Nairobi siku ya Alhamisi, huku magari yakichomwa moto na polisi wakirusha vitoa machozi kutawanya waandamanaji waliokasirishwa na kifo cha mwanablogu akiwa mikononi mwa polisi wiki iliyopita.
Kifo cha Albert Ojwang mwenye umri wa miaka 31, ambaye alikuwa anaandika kuhusu masuala ya siasa na kijamii, ni cha hivi karibuni kuangazia vyombo vya usalama, ambavyo vimelaumiwa kwa kuwaua watu kiholela na watu kutekwa kwa miaka kadhaa.
Polisi walitumia vitoa machozi kutawanya mamia ya waandamanaji katika mji mkuu, ambapo magari yasiyopungua mawili yalichomwa moto, siku moja baada ya Rais William Ruto kusema kuwa Ojwang aliuawa akiwa "mikononi mwa polisi", akifuta taarifa zilizokuwa zimetolewa awali kuhusu kifo chake.
Awali polisi walisema kuwa Ojwang alikamatwa magharibi mwa Kenya siku ya Ijumaa kwa madai ya kumharibia sifa afisa mmoja mwandamizi wa polisi mtandaoni na kufariki ‘‘baada ya kugonga kichwa chake ukutani akiwa ndani ya seli".
Wito wa uchunguzi
Mamlaka huru ya kusimamia utendakazi wa polisi imeanzisha uchunguzi, huku Umoja wa Ulaya na Marekani wakitoa wito wa kufanyika uchunguzi wa wazi kuhusu kifo cha mwanablogu huyo.
Siku ya Alhamisi waandamanaji walitaka afisa mwandamizi wa polisi ajiuzulu wakidai amehusika na kifo cha Ojwang, huku wengine wakiwa wamebeba bendera za Kenya.
Majeraha ya mwanablogu huyo, ikiwemo majeraha ya kichwa, shingoni, yameonesha kuwa aliteswa kabla ya kuuawa, kwa mujibu wa mwanapatholojia Bernard Midia, ambaye alikuwa sehemu ya madaktari waliofanya upasuaji wa maiti.
Siku ya Jumatano, Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja aliomba radhi kwa polisi kutoa taarifa za kupotosha zilizosema kuwa Ojwang alijiuwa.
"Kulingana na ripoti ya IPOA ... siyo kweli... Hakujigonga na ukuta," Kanja aliliambia bunge la Seneti.