AFRIKA
2 dk kusoma
Serikali Uganda yasema iko tayari kusambaza umeme kuanzia Aprili 2025
Baada ya miongo miwili ya kutoa huduma ya usambazaji wa umeme Uganda, kampuni ya UMEME inalazimika kusitisha shughuli za usambazaji wake nchini humo.
Serikali Uganda yasema iko tayari kusambaza umeme kuanzia Aprili 2025
Kampuni ya kusambaza umeme nchini Uganda inafunga oparesheni zake baada ya miaka 20/ picha UMEME / Public domain
19 Machi 2025

Kuanzia Aprili 2025, Kampuni ya Usambazaji Umeme ya Uganda itachukua udhibiti wa kampuni ya kusambaza umeme inayoitwa UMEME Limited, kampuni kibinafsi ambayo imekuwa ikisambaza umeme kote nchini.

Baada ya miongo miwili ya kutoa huduma ya usambazaji wa umeme Uganda, kampuni hiyo inalazimika kufunga oparesheni zake nchini humo.

Imeongeza usambazaji kutoka watu laki mbili hadi milioni mbili na laki mbili.

“Tunatoa uhakikisho wa serikali kuchukua jukumu la usambazaji wa Umeme,” Wizara ya Nishati imesema katika taarifa yake.

Hata hivyo, Ziria Tibalwa ambae ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Umeme (ERA) ametilia shaka utayari wa Serikali kuchukua nafasi ya Umeme Aprili 2025, akitaja ucheleweshaji wa Serikali kupata uwekezaji wa Dola za Kimarekani Milioni 50 unaohitajika na Kampuni ya Usambazaji Umeme ya Uganda kama uwekezaji wa awali.

“Hatuko tayari hata kwa dola milioni 50 kwa UEDCL ya kuanza, hata mkataba wa makubaliano ambao haungeruhusu UEDCL kuingilia kati haiko tayari,” alisema Ziria Tibalwa, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Umeme (ERA).

Aliyasema hayo alipokuwa mbele ya Kamati ya Bunge ya Uchumi ya Kitaifa, wakati wa ukaguzi wa mkopo wa dola za Marekani Milioni 190 kutoka Benki ya Stanbic Uganda, kwa ajili ya ununuzi wa Umeme Limited.

Lakini Wizara ya Nishati katika taarifa yake imesema fedha zitapatikana.

“Wizara ya Fedha inaendelea kutafuta mbinu za kupata dola milioni 50 zinazohitajika kupitia mikopo ya ndani ya nchi,” imesema Wizara hiyo.

Watu kupoteza ajira

Waziri wa Nishati wa Uganda Ruth Nankabirwa amefichua kuwa ni jambo lisiloepukika kwa baadhi ya watumishi wa kampuni ya UMEME Limited kupoteza ajira baada ya serikali kuchukua majukumu ya usambazaji wa umeme.

Kufikia mwisho wa 2022, kampuni ya UMEME ilikuwa na wafanyakazi wa kudumu 2300 bila kujumuisha wale wanaofanya kazi kwa msingi wa mikataba ya muda mfupi. Ilikuwa na wafanyakazi wapatao 800 wenye mikataba.

Amesema hii lazima ifanyike ikiwa baadhi ya majukumu yanayotolewa na watumishi wa sasa wa kampuni ya UMEME tayari yanatekelezwa na wafanyakazi wa Kampuni ya Usambazaji Umeme ya Uganda (UEDCL).

"Wafanyakazi wa UMEME maombi yao yalikataliwa…tukiwahoji wote wawili, yule wa UMEME na UEDCL, mmoja wao atashindwa kwa hiyo jambo hili haliepukiki,” alisema Nankabirwa.

Waziri wa Nishati Ruth Nankabirwa alilihakikishia taifa kwamba Wizara ya Fedha imepata dola milioni 50 zinazohitajika kwa shughuli za Uganda Electricity Distribution Company Limited kuchukua jukumu la usambzaji wa umeme.

CHANZO:TRT Afrika
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us