Mfumo wa miaka mingi wa “misaada kutoka nje”, pale ambapo mataifa tajiri yanasaidia nchi maskini, sasa unaporomoka. Watu wanaonekana hawajali kuhusu hili. Je, haya si matumizi mabaya ya fedha? Na kwa nini walipa kodi wa nchi nyingine walipe kuwasaida watu sehemu ya mbali zaidi? Je misaada kwa mataifa ya nje siyo njia ya kuendeleza ukoloni kwa kutumia mbinu tofauti?
Kushindwa kutoa misaada kwa mataifa ya nje ni mkosi mkubwa, siyo tu kwa nchi maskini, bali kwa nchi ambazo zinasitisha misaada hiyo. Na hii ndiyo sababu.
Historia
Tuangalie tarakimu hizi. Katika siku yake ya kwanza akiwa Rais wa Marekani, Donald Trump alisitisha misaada yote ya Marekani kwa mataifa ya nje, na sasa inasemekana kuwa ni chini ya asilimia 10 pekee ndiyo watafanikiwa kupata tena misaada hiyo. Hili limeanzisha vurugu kila mahali. Uholanzi nayo ikafwata kwa kutangaza kupunguza asilimia 30 kwa fedha inazotoa kama misaada. Sasa, Uingereza imetangaza kupunguza kwa asilimia 40. Ufadhili wa nchi hizi tatu pekee utapunguza robo ya misaada inayotolewa duniani.
Haifahamiki kama huu ndiyo utakuwa mwisho. Ujerumani na Japan ndiyo wafadhili wakubwa waliobaki kwa sasa, lakini tayari wanasiasa wanataka matumizi yapunguzwe.
Si vigumu kufahamu kwa nini misaada hii inapunguzwa. Mataifa tajiri yana madeni mengi, na matatizo ya kwao wenyewe. Wapiga kura wao wanawachagua watu ambao watazingatia maslahi ya taifa lao kwanza. Wanaona misaada ya nje kama hisani ambayo haiwasaidii wao, na pia kama ubadhirifu na ufisadi.
Msaada kutoka nje siyo suluhu, lakini unaweza kusaidia nchi zinazotoa na nchi zinazopokea, na wafadhili wenyewe pia. Ni wakati sasa wa kuangalia itikadi za kupotosha.
Sababu milioni Kumi na saba
Hamna shaka kuwa baadhi ya misaada kutoka nje inafanyiwa ubadhirifu. Inatumiwa zaidi kwa malengo ya kisiasa kuliko kuwasaidia watu, kwa mfano kuwahonga Rwanda ili wawape makao wakimbizi ambao hawatakiwi. Lakini kuna baadhi ya maeneo ambayo matumizi ya misaada ya nje yamesaidia sana, na kumekuwa na matokeo mazuri.
Gavi ni shirika ambalo mataifa mengi hisani inalipa kwao, na linasaidia kupata chanjo kwa nchi ambazo hazina uwezo wa kupata chanjo hizo. Imebainika kupitia utafiti wa kitaaluma wa muda mrefu kuwa imeokoa maisha ya watoto milioni kumi na saba katika kipindi cha miongo miwili iliyopita. Hiyo ni zaidi ya vifo vya jumla katika vita vya kwanza vya dunia, na kwa gharama ya dola elfu moja tu kwa kila maisha ya mtu mmoja yaliyookolewa.
Lakini kwa nini walipa kodi wa Uingereza au Japan walipie gharama hizo?
Pamoja na kuwa masiha yanakuwa magumu pia kwa watu wanaoishi nchi tajiri, bado tunaishi katika dunia mbili tofauti. Zaidi ya watu bilioni moja wanaishi katika mataifa ambayo matumizi ya mwaka mzima kwa huduma ya afya ya mtu ni chini ya dola $100. Kiwango hicho hata hakitoshi kwenda kumuona daktari barani Ulaya, bado hapo hatujazungumzia matibabu kwa maradhi mazito.
Pamoja na kuwa misaada ya mataifa ya nje ni chini ya asilimia moja ya bajeti za nchi nyingi wafadhili, inasadia kwa kiasi kikubwa matumizi ya sekta ya afya kwa nchi kadhaa barani Afrika.
Faida za uwekezaji kwa wafadhili
Lakini kuokoa maisha yote hayo ni njia nzuri ya uwekezaji kwa wafadhili. Wanaweza kusaidia katika matatizo yote makubwa ambayo mataifa tajiri yanakabiliana nayo : migogoro, wahamiaji wasiyo halali na ukuaji wa uchumi.
Kwanza, tuangalie migogoro. Shirika la ujasusi la Marekani CIA lilifadhili utafiti wa kufahamu sababu ya kihistoria ya kuanzishwa kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe. Hawakufanya hivi kwa sababu ya kujitolea. Ilikuwa ni kuhusu usalama wa Marekani. Walibaini kuwa suala linalosababisha kwa kuanguka kwa serikali ni idadi ya watoto wanaofariki kutokana na maradhi kabla ya kutimiza umri wa miaka mitano — suala ambalo shirika la Gavi linalifanyia kazi kuliepuka. Tafiti zingine zimebaini kuwa misaada ya nje inaweza kupunguza hatari ya vita kurejea baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano.
Vipi kuhusu uhamiaji? Mwanauchumi kutoka taasisi ya Kiel, wakati akichambua suala la uhamiaji kote barani Afrika, amebaini sababu mbili kuu kwa watu kuhama kutoka maeneo ya migogoro, na ukosefu wa huduma za msingi kama vile ya afya. Ukifanikiwa kuimarisha huduma ya afya,unaokoa maisha, hakutakuwa na migogoro, na hivyo kupunguza uwezekano wa watu kutaka kuhama.
Faida ya tatu ni kukuwa kwa uchumi. Wafadhili kama Ujerumani na Japan wanauza idadi kubwa ya magari nje ya nchi zao, pamoja na teknolojia na bidhaa zingine, lakini ukuaji wao umepungua kasi. Kupata soko jipya kwa ajili ya bidhaa zao kutasaidia sana. Lakini mataifa mengi barani Afrika ni maskini. Kulingana na tafiti nyingi za kitaaluma, jambo lilochangia umaskini ni magonjwa ambayo shirika la Gavi na miradi mingine inayofadhiliwa na nchi za nje inajitahidi kuangamiza.
Ushirikiano, siyo ufadhili wa mashaka
Na vipi kuhusu shutma kuwa misaada kutoka mataifa ya nje ni mbinu mpya ya ukoloni ikionesha kuwa wazungu ndiyo wanasaidia ? inawezekana, lakini siyo lazima iwe hivyo.
Korea Kusini lilikuwa taifa maskini sana, lilotawaliwa na wakoloni, na baadaye likawa nchi tajiri. Na sasa ni mfadhili mkubwa, kwa sababu raia wa Korea walithamini msaada waliopata kutoka kwa Marekani na mataifa mengine kipindi wakijaribu kujiimarisha. Msaada wao unajikita zaidi katika ushirikiano wala siyo ubabe.
Mataifa ya Mashariki ya Kati kama Uturuki, Saudi Arabia, Imarati na Qatar pia ni miongoni mwa wafadhili wakubwa, wote kutokana na kuungana na majirani, lakini pia kuimarisha ushawishi wao na miungano.
Mara nyingi wafadhili hawa wasio wazungu wameliangazia suala la misaada ya kigeni kama uhusiano kati ya mataifa yaliyo sawa, ambapo taifa tajiri halioneshi ubabe wowote. Na mataifa ya wazungu pia yameanza kuiga mfano huu, kuna baadhi ya mataifa ambayo hayaendekezi mfumo mwingine wowote.
Na ndiyo maana kila mara Rais wa Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amekuwa akiutaja ushirikiano wa Umoja huo na Afrika kama “ushirikiano wa usawa”.
Misaada kutoka nje bado yana mapungufu. Yana mitazamo ya kikoloni. Na siyo suluhisho kwa kila tatizo. Haiwezi kusitisha vita, kuzuia uhamiaji haramu au kufanya Swaziland iwe na uchumi kama wa Uswizi.
Lakini inaweza kusaidia na matatizo makubwa matatu ya nchi tajiri, huku ikiokoa maisha watu wengi zaidi. Kuna njia mbaya zaidi za matumizi ya pesa za serikali.