Rais wa Marekani Donald Trump alitishia kusitisha ufadhili wa serikali kuu kwa jiji la New York ikiwa mteule wa meya wa chama cha Democratic Zohran Mamdani "hatafanya jambo sahihi" kama meya.
Trump alitoa onyo hilo wakati wa mahojiano na shirika la habari la Fox News siku ya Jumapili, yakimlenga Mamdani, ambaye alipata uteuzi wa Meya wa Kidemokrasia mnamo Juni 24.
"Ikiwa atashinda, nitakuwa rais, na itabidi afanye jambo sahihi, la sivyo hawatapata pesa yoyote. Ni lazima afanye jambo sahihi," Trump alisema.
Alitoa tishio lake kwa meya yeyote wa baadaye wa New York, akisema: "Yeyote ambaye atakuwa meya wa New York atalazimika kujirekebisha, au serikali ya shirikisho itawashinikiza sana kifedha."
Hapo awali Trump alitishia majimbo na vyuo vikuu kadhaa kuzipunguzia ufadhili wa serikali ikiwa hazitazingatia sera zake.
Alimwita Mamdani "mkomunisti" na alionyesha kushtushwa na uwezekano wake wa kuchaguliwa meya wa mji wa New York.
"Yeye ni mkomunisti. Nadhani ni mbaya sana kwa New York," alisema.
"Inashangaza," alisema na kuongeza: "Nilikuwa nikisema hatutakuwa na mtu mwenye siasa za kiujamaa katika nchi hii, lakini sasa tutakuwa na mkomunisti."
Mamdani, ambaye alizaliwa Uganda, alimshinda gavana wa zamani wa New York Andrew Cuomo katika mchujo wa Jumanne, akijiweka nafasi ya kuwa meya wa kwanza Muislamu wa Jiji la New York.
Mgombea huyo wa chama cha Democratic amekuwa akiunga mkono sana Palestina na mkosoaji wa Israel.
Alikuwa mwanzilishi mwenza wa uwanaharakati wa wanafunzi katika kutetea haki Palestina katika chuo cha Bowdoin na mnamo 2023 alijiunga na mgomo wa kukaa na njaa nje ya Ikulu ya White House akitaka kusitishwa kwa mapigano huko Gaza.