Simulizi mbalimbali za kumuhusu Papa huyu zimetamalaki, zikipamba kurasa mbalimbali kwa sasa.
Ibada mbalimbali Misa za Ukumbusho zinasikika kote, ndani ya makanisa madogo na hata makubwa, mijini na mashambani; kote wamekusanyika kwa ukimya mkuu huku bendera zikipepea nusu mlingoti.

Kanisa katoliki linaomboleza kifo cha kiongozi wake Papa Francisco.
Ni maombolezo kwa mtu aliyeacha wosia wa kutohitaji mazishi ya kifahari, kama ilivyokuwa kwa watangulizi wake, isipokuwa eneo la kanisa la Mtakatifu Maria Maggiore, sehemu aliyopenda kufanyia ibada na sala kwa heshima ya Bikira Maria.
“Kaburi lazima liwe kwenye ardhi; la kawaida, bila mapambo maalum,” aliandika.
Akaongeza: Liwe na jina langu tu. Franciscus.
‘Sede vacante’, kiti ki wazi
Kwa kipindi hichi, Kanisa Katoliki limeingia kwenye kipindi cha ‘Sede Vacante’, yaani kiti cha uongozi kipo wazi kufuatia kifo cha Papa Francis, kilichotokea Aprili 21, 2025.
Kiti cha Mtakatifu Petro hakina mtu huku pete yake, maarufu kama ‘Pete ya Mvuvi’ ikiharibiwa na afisa mwandamizi ndani ya Vatican, maarufu kama Camerlengo, kuashiria mwisho wa enzi ya Papa huyo.
Tayari, kiongozi huyo aliandaaa mazishi yake akiondoa chembechembe za utamaduni uliokuwepo.
Mwili huo utalazwa ndani ya Basilica ya Mtakatifu Petro kwa unyenyekevu wote.
Jeneza la kawaida
Hapatakuwa na sherehe yoyote, huku Rogito ambao ni wasifu wake ukisomwa hadharani kisha kufungiwa ndani.
Mazishi hayatahusisha mataji na uvumba. Yatakuwa ya unyenyekevu mkubwa. Aliongoza Kanisa Katoliki duniani kwa miaka 12, akiongoza kwa mfano.
Alikataa mavazi ya dhahabu, akatembea bila walinzi, akafungua milango ya Vatican kwa wahamiaji na waliodharauliwa.
Katika wosia wake wa mwisho, maziko ya kawaida kabsia; sala, jeneza la mbao, na kukumbukwa kama “mwenye dhambi aliyekombolewa.”
Katika utangulizi wa kitabu cha Kardinali Angelo Scola, aliandika: “kifo sio mwisho wa kila kitu, bali ndiyo mwanzo wa kitu.”
Jumuiko La Makardinali
Mazishi yatakapokwisha Jumamosi, mila nyingine inaanza.Makadinali, walioapa usiri, wanaingia kwenye Sistine Chapel chini ya mtazamo mkali wa Hukumu ya Mwisho ya Michelangelo. Wanapiga kura.
Mara mbili asubuhi. Mara mbili tena mchana. Vikaratasi. Vimekunjwa. Vimetiwa alama. Vimechomwa. Moshi mweusi ishara ya kushindwa.
Moshi mweupe - mafanikio.
Na wakati unapowadia, kengele za Mtakatifu Petro zitasikika.
Utamaduni wa muda mrefu.
Ulimwengu wote uta paza macho kwenye sakafu.
Pazia litafunguka.
Na kiongozi wa Makardinali atajitokeza kwenye lile dirisha maarufu na kutamka maneno haya: Habemus Papam, yaani tumepata Papa.