Marekani imetangaza kuwa viza za wanamziki wa mtindo wa punk wa Uingereza Bob Vylan zimebatilishwa kufuatia nyimbo yao ya "Death to the IDF (jeshi la Israel)" wakati wa Tamasha la Glastonbury.
"Wizara ya Mambo ya Nje imebatilisha viza za Marekani kwa wanamziki wa bendi ya Bob Vylan kutokana na chuki zao huko Glastonbury, ikiwa ni pamoja na kuongoza umati katika nyimbo za vifo," Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Christopher Landau aliandika kwenye mtandao wa X siku ya Jumatatu.
"Wageni wanaofurahia vurugu na chuki hawakaribishwi katika nchi yetu."
Hatua hiyo imekuja baada ya wanamziki wa kundi hilo kuimba "Death to the IDF" na "Free, Palestine Free" wakati wa tamasha lao la Jumamosi huko Glastonbury, tamasha kubwa la muziki la Uingereza.
Hapo awali, afisa wa Wizara ya Mambo ya Nje alisema wanaangalia ubatilishaji huo, akisema "serikali ya Marekani haitatoa viza kwa mgeni yeyote anayeunga mkono magaidi."
Muimbaji wao mkuu, ambaye anajulikana kwa jina la kisanii Bobby Vylan, alionekana kuongoza mashabiki kwenye tamasha la wikendi katika picha kwenye mtandao wa Instagram, akiandika: "Nilisema nilichosema."
"Kufundisha watoto wetu kutetea mabadiliko wanayotaka na kuhitaji ndiyo njia pekee ya kufanya ulimwengu huu kuwa mahali pazuri," aliongeza.
Uingereza yaanzisha uchunguzi wa uhalifu
Baada ya tangazo hilo la Marekani, polisi wa Uingereza pia walisema wanaanzisha uchunguzi wa uhalifu kuhusu utendakazi huo.
Polisi walisema walifanya uamuzi huo baada ya kukagua kanda za video na sauti za mziki huo.
Israel imewaua zaidi ya Wapalestina 56,500, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, hadi sasa katika eneo lililozingirwa la Gaza.
Takriban Wapalestina 11,000 wanahofiwa kufukiwa chini ya vifusi vya nyumba zilizoharibiwa, kulingana na shirika rasmi la habari la Palestina WAFA.
Wataalamu, hata hivyo, wanadai kwamba idadi halisi ya vifo inazidi kwa kiasi kikubwa na ile inayotolewa na mamlaka ya Gaza, na kukadiria kuwa inaweza kuwa karibu 200,000.
Katika kipindi cha mauaji ya kimbari, Israel iligeuza sehemu kubwa ya eneo lililozingirwa kuwa magofu na kuwahamisha watu wote.
Novemba mwaka jana, Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC ilitoa hati za kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Waziri wake wa zamani wa Ulinzi Yoav Gallant kwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu huko Gaza.
Israel pia inakabiliwa na kesi ya mauaji ya halaiki katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki kwa vita vyake dhidi ya eneo hilo.