Maisha
4 dk kusoma
Hii ni Kwaresima
Ikiwa imetoholewa kutoka neno la Kilatini ‘Quadragesima’ lenye maana ya 40, kipindi cha Kwaresima ni siku 40 za hija ya kiroho.
Hii ni Kwaresima
Siku hizo 40 hutanguliwa na Jumatano ya majivu, ambapo Wakristu hasa wa madhehebu ya Katoliki hupakwa majivu kwenye paji la uso kama ishara ya kukumbushwa kufanya toba, pia kuwa wanadamu ni mavumbi tu na siku moja watarudi mavumbini, hivyo kutilia umuhimu wa kubadilisha mwenendo wa maisha yao.
5 Machi 2025

Tubuni na kuiamini Injili.

Ni maneno yatakayotawala vinywa vya makasisi ndani ya Makanisa ya Kikristo ulimwenguni kote siku ya Machi 5, wakati wa kuanza kwa kipindi cha Kwaresima.

Ikiwa imetoholewa kutoka neno la Kilatini ‘Quadragesima’ lenye maana ya 40, kipindi cha Kwaresima ni siku 40 za hija ya kiroho.

Ni kipindi ambacho Wakristo hukumbuka siku 40 ambazo Yesu Kristo alitumia akiwa jangwani, akijaribiwa na shetani, kama ilivyoandikwa kwenye vitabu Vitakatifu.

Waumini wa Kikristo hutumia kipindi hicho kusali, kufunga, kufanya toba na kufanya matendo ya huruma kwa wahitaji.

Siku hizo 40 hutanguliwa na Jumatano ya majivu, ambapo Wakristu hasa wa dhehebu la Katoliki hupakwa majivu kwenye paji la uso kama ishara ya kukumbushwa kufanya toba, pia kuwa wanadamu ni mavumbi tu na siku moja watarudi mavumbini, hivyo kutilia umuhimu wa kubadilisha mwenendo wa maisha yao.

Kwaresma huhitimishwa na Juma Kuu, ambalo huanza na Alhamisi Kuu, Ijumaa Kuu, Jumamosi Kuu na kisha Pasaka ambapo Wakristu huadhimisha ufufuko wa Yesu Kristo baada ya mateso yake siku ya Ijumaa Kuu.

“Kanisa huanza kipindi cha Kwaresima kwa ibada ya Jumatano ya Majivu, kielelezo cha toba na wongofu wa ndani. Hiki ni kipindi cha sala na kufunga; kusoma na kulitafakari Neno la Mungu,” anaeleza Padre Ngapemba Tinga, kutoka Jimbo Kuu la Dar es Salaam, ambaye kwa sasa yuko masomoni Roma nchini Italia.

Safari ya jangwani

Kwa mujibu wa Padre Tinga, Kwaresima ni kipindi rasmi kinachoakisi siku 40 ambazo Yesu alisali na kufunga jangwani huku alijaribiwa na shetani kabla ya kuanza rasmi mafundisho yake kwenye jamii.

 Ni kipindi muhimu cha maandalizi ya Pasaka, ambayo ni kumbukumbu ya mateso, kifo na ufufuko wa Yesu Kristo, kama ilivyoandikwa na Wainjili Marko, Matayo na Luka.

“Kwaresima ni kipindi chenye historia ndefu juu ya imani, utamaduni na mafudisho ya wakristu wa mwanzo. Miaka 200 baaada ya Kifo na ufufuko wa Yesu, wakristu waumini walipokea imani katika namna mbalimbali kadiri ya tamaduni, mila, desturi na mabadiliko ya nyakati zao. Walikuwa wana namna mbalimbali ya kusali na kuenzi Imani yao. Wakristu walitenga siku tatu za sala, tafakari na mfungo,” anaeleza Padre Tinga katika mahojiano yake na TRT Afrika.

Kwa upande wa wakristu Wakatoliki, Kwaresima ni kipindi muhimu kwa waamini kujiweka karibu zaidi na Kristo Mfufuka, kama ilivyowahi kusemwa na Baba Mtakatifu Fransisko katika moja ya mahubiri yake wakati wa mfungo wa Kwaresima.

“Hiki ni kipindi cha kufunga. Kufunga katika dini nyingi inachukuliwa kama aina ya kujitesa na kujinyima na hata wengine kipindi hiki utasikia wakisema wanalala chini bila godoro au wanazima simu zao au mitandao ya kijamii au wanajikatalia kula nyama au kunywa bia au mvinyo au hata soda, na mambo mengi mengine watu wanajikatalia katika kipindi cha Kwaresma,” anaandika Padre Gaston George Mkude kwenye mtandao wa Vatican, akiwa Roma.

 Asili ya namba 40

Namba 40 inabeba maana ya kiteolojia zaidi kuliko kuchukuliwa kama muda tunaoweza kuuhesabu kama tunavyoweza kufanya sasa kwa kuupima.

Namba hiyo huwakilishwa kipindi kirefu au muda wote wa maisha. Pia ni muda wa matayarisho kwa ajili ya jambo muhimu na kubwa katika siku za usoni.

Kwa mfano, mafuriko ya Nuhu yalidumu siku 40, miaka 40 Wanawaisraeli walisafiri jangwani kabla ya kuingia nchi ile ya ahadi, siku 40 watu wa Ninawi walifanya toba ya kufunga, na ndivyo kwa Eliya, Musa na Yesu kwa siku 40.

“Na ndio Kanisa la awali likaona pia umuhimu wa kutenga siku 40 kama siku za matayarisho kwa ajili ya kilele mama ya sikukuu zote yaani Pasaka. Na ndizo siku 40 za mfungo, sala na matendo mema kama matayarisho ya Pasaka yaani Kwaresima,” anaeleza Padre Tinga.

Kulingana na Kasisi huyo, Kanisa limetenga kipindi cha Kwaresima kwa ajili ya kufanya mambo makuu matatu yaani, Sala, Kufunga na Kutenda Mema, yote ikiwa na shabaha ya kufanya toba na mabadiliko ya kweli ya ndani, kubadili vichwa na namna za watu kutenda na kufikiri.

“Ni kipindi cha kufanya mabadiliko, ni kipindi cha kufanya metanòia, yaani mabadiliko katika maisha. Ni kipindi cha neema, cha mageuzi na mapinduzi ya kweli ndani mwetu, katika maisha yetu, katika safari yetu kumwelekea Mungu,” anasisitiza Kasisi huyo.

Kujinyima

Mbali na kuzama katika sala, kipindi cha Kwaresima ni wakati wa kufunga, wakati wa kujisahau na kuachana na ubinafsi kwa ajili ya wengine, hasa wale wahitaji.

“Kufunga kwetu hakutokuwa na maana ikiwa tutashinda tuu njaa na kiu kama kile tunachojikatalia hakiendi kumsaidia mwingine aliye muhitaji; funga yetu ni mwaliko wa kuwaza na kutenda kama Mungu, ni mwaliko wa kuwa wakarimu zaidi kwa wengine wanaokuwa katika uhitaji,” anahitimisha Padre Tinga.

CHANZO:TRT Afrika Swahili
Tazama TRT Global. Shiriki maoni yako!
Contact us