ULIMWENGU
2 dk kusoma
Mkenya Jamal Ahmed kuongoza udhibiti wa Polio WHO
Dkt. Ahmed anatambuliwa kwa juhudi zake kwenye shirika hilo katika miradi ya kuangamiza ugonjwa wa kupooza akiwa Geneva na Pakistan.
Mkenya Jamal Ahmed kuongoza udhibiti wa Polio WHO
Utaalamu wa Dkt Ahmed ni katika mifumo ya ufuatiliaji, WHO inasema. / TRT Afrika English
13 Machi 2025

Shirika la afya Duniani (WHO) limemteua Dkt. Jamal Ahmed, daktari kutoka Kenya kuwa mkurugenzi wa idara ya kuangamiza ugonjwa wa kupooza..

WHO inasema Dkt Ahmed analeta uzoefu wa kipekee kwenye wadhifa huo, baada ya kuwa mratibu shirika hilo barani Afrika katika mradi wa kuangamiza polio tangu 2022.

"Dkt Ahmed anaingia kwenye nafasi hii muhimu ya kuangamiza polio, kufuatia kifo cha aliyekuwa mkurugenzi Aidan O’Leary Agosti 2024," WHO ilisema.

Ahmed pia anafahamika kwa kuwa katika nafasi muhimu za miradi ya kuangamiza ugonjwa wa kupooza mjini Geneva na nchini Pakistan, akiangaza ufuatiliaji, uwezo wa kupima, na uchanganuzi wa data.

‘Tutaimaliza kazi’

"Nimefurahi sana kwa uteuzi huu wa Mkurugenzi wa mradi wa kuangamiza Polio WHO. Tunafahamu kuwa maendeleo yamekuwa yakibadilika, tutakabiliana na changamoto hizi kwa kutumia mifumo ya uchanganuzi, ari, na mtazama chanya kumaliza kazi hii. Nawashkuru sana kwa kuniamini," Dkt Ahmed aliandika kwenye ukurasa wake X.

Amefanya katika kituo cha kudhibiti magonjwa (CDC) mjini Nairobi, akiangazia wakimbizi na msaada wa kiafya kote Afrika Mashariki, na katika shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na masuala ya wakimbizi (UNHCR) nchini Jordan na Uswizi.

Uzoefu wa Dkt Ahmed uko zaidi katika mifumo ya ufuatiliaji, kuimarisha upimaji, ujumuishaji wa jamii, na kuhakikisha vijana na kina mama wana kauli katika masuala ya afya. Amesomea shahada ya udaktari nchini Uturuki na shahada ya uzamili kutoka Uingereza.

Uteuzi wa Dkt Ahmed umekuja wakati muhimu sana, huku WHO ikitangaza maambukizi mapya 134 ya ugonjwa wa kupooza katika nchi zisizopungua saba 2024.

WHO inasema polio inaathiri zaidi watoto wa chini ya umri wa miaka 5, huku mmoja kati ya watoto 200 akipooza kabisa katika umri wake wote.

Ugonjwa huu ambao unaambukiza kwa haraka unasababishwa na virusi kwenye mfumo wa ubongo na inaweza kumfanya mtu akapooza katika kipindi cha saa chache. Virusi hivi husambazwa kupitia maji au chakula.

 

CHANZO:TRT Afrika
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us