Bunge lililoteuliwa na serikali ya kijeshi ya Mali siku ya Alhamisi limempa kiongozi wa kijeshi wa nchi hiyo muhula wa miaka mitano madarakani, unaoweza kufanywa upya zaidi ya mara moja na bila kuchaguliwa, Shirika la AFP limeripoti.
Assimi Goita alichukua uongozi 2020 baada ya kufanya mapinduzi ya serikali. Amehudumu kama Rais wa mpito wa Mali tangu 2021.
Uamuzi wa sasa wa bunge unafungua njia kwa Jenerali Assimi Goita kuiongoza nchi hiyo ya Magharibi mwa Afrika hadi angalau 2030, licha ya ahadi ya awali ya serikali ya kijeshi kurejea katika utawala wa kiraia Machi 2024.
Muswada huo ulipitishwa na Baraza la Kitaifa la Mpito, ambalo linajumuisha wanachama 147, na sasa unaenda kwa mkuu wa jeshi mwenyewe ili kutiwa saini rasmi. Baraza la Mawaziri lilikuwa tayari limepitisha hatua hiyo mwezi uliopita.
Kuvunja ahadi
Goita alipoingia madarakani kufuatia mapinduzi mawili mwaka 2020 na 2021, alisisitiza kujitolea kwa Mali katika mapambano dhidi ya makundi ya waasi na awali aliahidi kuirejesha katika utawala wa kiraia.
Lakini jeshi hatimaye lilikaidi ahadi yake ya kuachia madaraka kwa raia waliochaguliwa kufikia tarehe ya mwisho ya Machi 2024.
"Hii ni hatua kubwa mbele katika ujenzi wa Mali," Malick Diaw, rais wa Baraza la Kitaifa la Mpito, aliiambia AFP baada ya kura ya Alhamisi.
Vyama vya siasa vimepigwa marufuku
Tangu mwaka 2012, Mali imekumbwa na ghasia zinazotekelezwa na makundi ya waasi yenye uhusiano na ugaidi.
Mashambulizi hayo yameongezeka katika wiki za hivi karibuni.
Mapema mwaka huu, bunge la kitaifa lililoundwa na jeshi lilipendekeza hatua ya kumtangaza Goita kuwa rais bila kupigiwa kura kwa muhula wa miaka mitano unaoweza kufanywa upya.
Mkutano huo pia ulipendekeza kufutwa kwa vyama vya siasa, ambavyo serikali ya utawala ilipiga marufuku mwezi Mei.