Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amezungumzia kuhusu hali ya uchumi wa nchi yake katika kikao cha bunge, jijini Addis Ababa.
Abiy Ahmed amesema Ethiopia ni nchi yenye uwezo mkubwa wa madini barani Afrika lakini kwa miaka mingi, sekta hiyo ilikosa uongozi makini na dira ya wazi ambayo ingeweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika uchumi wa taifa.
“Leo, tunafanya kazi ili kubadilisha hiyo. Mwaka jana, Ethiopia iliuza nje tani 37 za dhahabu. Mwaka huu, kutokana na juhudi endelevu na umakini wa kimkakati, tulipata thamani ya mauzo ya nje isiyokuwa ya kawaida ya dola bilioni 3.5,” Ahmed aliwaambia wabunge.
“Katika sekta ya gesi, maendeleo yalikuwa yamekwama kwa muda mrefu kwani makampuni hayakuweza kupata leseni na kuanza kufanya kazi. Hiyo sasa inabadilika. Hivi karibuni Ethiopia itaanza kuuza bidhaa zake za gesi, kuonyesha kwamba sisi sio tu wamiliki wa rasilimali lakini washiriki hai,” aliongezea.
Waziri Mkuu huyo pia ameeelezea kuwa zaidi ya hayo, ujenzi wa kiwanda kikubwa cha mbolea unatarajia kuanza hivi karibuni.
Mara tu itakapokamilika amesema kitafanya kazi kikamilifu ndani ya miezi 40, ikichukua jukumu muhimu katika kusaidia uzalishaji wa kilimo wa Ethiopia na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje.
Sekta ya viwanda
Kiwango cha ukuaji wa asilimia 12 kinalengwa kwa sekta ya viwanda nchini humo mwaka huu.
“Maendeleo makubwa yamepatikana chini ya Kampeni ya “Made in Ethiopia.” Mwaka jana, uwezo wa uzalishaji viwandani wa Ethiopia ulisimama kwa asilimia 59; mwaka huu, umeongezeka hadi asilimia 65—ikichangiwa zaidi na kuboreshwa kwa utendaji wa viwanda na utumiaji wa uwezo,” Waziri Mkuu Ahmed amesema.
“Uzalishaji wa saruji umeongezeka, na bidhaa za chuma zimerekodi ukuaji wa asilimia 18. Ethiopia pia imejenga uwezo wa uzalishaji wa chuma, na kazi inaendelea ili kukidhi mahitaji ya ndani kikamilifu. Kiwanda kikubwa cha vioo, chenye uwezo wa uzalishaji wa kila mwaka wa karibu tani 600,000, kinajengwa kwa sasa,” ameongezea.
Kiwanda hicho cha vioo kinatarajiwa kukamilika Disemba mwa huu au Januari 2026.
Aidha, amesema viwanda vya kuzalisha umeme wa jua vinatengenezwa na vitazinduliwa hivi karibuni. Juhudi hizi zinaonyesha dhamira yetu inayoendelea ya kufufua na kubadilisha msingi wa viwanda wa Ethiopia.
Sekta ya kilimo
Kilimo kinasalia kuwa uti wa mgongo wa uchumi wa Ethiopia lakini bado nchi hiyo ni kati ya nchi zinazoripotiwa kutegemea usaidizi wa chakula kutoa mashirika ya misaada.
Sasa Waziri Mkuu Ahmed anasema serikali inataka kuongeza juhdu za uzalsihaji wa ndani wa chakula.
“Nchi ambayo haiwezi kujilisha yenyewe haiwezi kulinda mustakabali wake kikamilifu. Katika miaka ya hivi karibuni, raia milioni 27 walitegemea mpango wa usalama. Kupitia juhudi endelevu, milioni 23 kati yao wamefanikiwa kujitosheleza—ushuhuda wa wazi wa uthabiti na maendeleo ya Ethiopia,” alisema.
“Ni lazima sasa tuzingatie kuwawezesha wanaolengwa milioni 4 waliosalia na kuhakikisha kuwa Ethiopia inakuwa taifa ambalo limeafiki kikamilifu uhuru wa chakula. Kwa ardhi yetu kubwa ya kilimo na kujitolea kuendelea, lengo hili linaweza kufikiwa."