Muandamanaji anaweza kutozwa faini ya karibu dola 800 au kufungwa jela hadi miezi mitatu iwapo atapatikana na hatia ya kushiriki maandamano katika maeneo ambayo hayaruhusiwi.
Muswada huo wa marekebisho ya nidhamu ya umma, 2025, uliowasilishwa na mbunge Esther Passaris, unapendekeza maeneo ambayo waandamanaji hawatoruhusiwa kufanya mikutano ya hadhara au maandamano.
Kulingana na muswada huo, maeneo hayo ni pamoja na: mita 100 kutoka majengo ya bunge, maeneo yenye ulinzi mkali (kama vile Ikulu) na majengo ya mahakama.
Kama muswada huo utakuwa sheria, Waziri wa Mambo ya Ndani, kwa kushauriana na serikali ya kaunti, ataweza kutenga maeneo maalum katika miji mikubwa ambapo maandamano yatafanyika.
Hii inamaanisha kuwa waandamanaji wataruhusiwa tu kukusanyika katika maeneo maalum, na kama wana malalamiko yoyote, viongozi wao ndiyo watakutana nao.
Hata hivyo, baadhi ya wabunge tayari wameeleza wasiwasi wao kuhusu muswada huo, wakisema kuwa itakuwa vigumu kutekeleza sheria hiyo nchini Kenya.