Helikopta ya vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Afrika nchini Somalia ilianguka siku ya Jumatano katika uwanja wa kimataifa wa ndege katika mji mkuu,Mogadishu, afisa mmoja alisema.
Afisa wa sekta ya usafiri wa ndege mjini Mogadishu, ambaye hakutaka kutambulishwa kutokana na kutoruhusiwa kuzungumza na vyombo vya habari, ameliambia shirika la Anadolu kuwa helikopta hiyo ya walinda amani ilikuwa na maafisa wanane na ililazimika kutuwa kwa dharura katika uwanja wa ndege wa Aden Adde mjini Mogadishu baada ya kuondoka uwanja wa Balidoogle ambapo kuna wanajeshi wa Marekani na Somalia.
Alisema kuwa kuna watu waliofariki bila kutaja idadi ya waliouawa au waliojeruhiwa kwenye ajali hiyo, lakini akaongeza kuwa maafisa wa uokoaji na zimamoto walifika kwenye eneo hilo na kuuzima moto wa helikopta iliyopata ajali.
AUSSOM ina wanajeshi 11,000 nchini Somalia kusaidia jeshi la nchi hiyo kukabiliana na wapiganaji wa kundi la al-Shabaab.
Moshi mkubwa
Vikosi hivyo vinajumuisha wanajeshi kutoka nchi ya Uganda na Kenya.
Halima Ahmed, mkazi wa wilaya ya Wabari mjini Mogadishu aliyezungumza na Anadolu kwa njia ya simu, amesema aliona moshi mkubwa kutoka upande wa uwanja wa ndege siku ya Jumatano.
Ndege kadhaa zilichelewa kupaa na kutuwa kutokana na tukio hilo lakini kwa sasa hali inasemekana kurudi kama kawaida.