Wizara ya Sheria ya Marekani siku ya Alhamisi ilimtaka jaji kufuta shtaka la ulaghai dhidi ya kampuni ya ndege ya Boeing.
Kampuni hiyo inalaumiwa kwa ajali mbili mbaya za ndege ya 737 MAX iliyoua watu 346, Wizara ya Sheria ya Marekani inasema imefikia makubaliano na kampuni hiyo ya kutengeneza ndege.
Boeing mnamo Julai 2024 ilikiri shtaka la kula njama ya uhalifu baada ya ajali mbili mbaya za 737 MAX nchini Indonesia na Ethiopia kuanzia 2018 na 2019.
Mnamo 2023, Jaji Reed O'Connor huko Texas alisema "uhalifu wa Boeing unaweza kuzingatiwa kama uhalifu mbaya zaidi wa shirika katika historia ya Marekani."
Chini ya mpango huo, Boeing itaepuka kutajwa kama mhalifu aliyehukumiwa, lakini imekubali kulipa dola milioni 444.5 za ziada katika mfuko wa walioathiriwa na ajali hiyo ambazo zitagawanywa sawa kwa kila aliyethirika na ajali pamoja na faini ya ziada ya dola milioni 243.6.
Mkurugenzi Mtendaji wa Boeing Kelly Ortberg alitia saini makubaliano hayo siku ya Alhamisi, na kukamilisha makubaliano ambayo Wizara ya Sheria ilisema wiki iliyopita iliafikiwa kimsingi.
Wizara ya Sheria ilisema idadi kubwa ya familia za watu 346 waliouawa katika ajali hiyo wamemaliza kesi za madai na Boeing na kwa pamoja "wamelipwa dola bilioni kadhaa."
"Boeing imethibitisha kuzingatia majukumu yake chini ya azimio lililofikiwa leo, ambalo linajumuisha faini kubwa ya ziada na ahadi za kuimarisha zaidi taasisi na uwekezaji," kampuni hiyo ilisema Alhamisi.
Boeing, ambayo mwaka jana ilikiri kuwa na hatia kama sehemu ya makubaliano, italipa jumla ya dola bilioni 1.1, ikijumuisha faini na fidia kwa familia na zaidi ya dola milioni 455 ili kuimarisha uzingatiaji, usalama na mipango bora kwa kampuni, Wizara ya Sheria ilisema.
Makubaliano hayo yamekosolewa vikali na familia nyingi ambazo zilipoteza jamaa zao katika ajali hizo na kushinikiza waendesha mashtaka kuipeleka Boeing mahakamani.
Wakili wa wanafamilia na maseneta wawili wa Marekani walikuwa wameitaka wizara ya Sheria kutoachana na mashtaka yake na baadhi ya mawakili wameapa kupinga mpango huo.
Serikali ilisema mpango huo "unazingatia uwajibikaji wa uhakika, unatoa manufaa makubwa na ya haraka kwa umma, na unafikisha ukomo katika kesi ngumu ambayo matokeo yake yasingekuwa ya uhakika."
Chini ya makubaliano hayo, Boeing haitakabiliwa tena na suala la kufanyiwa tathmini au kufuatiliwa tena lakini itaajiri mshauri wa kuwafuatilia.
Kama masharti ya mpango huo, bodi ya wakurugenzi ya Boeing itahitajika kukutana na familia za waliofariki kwenye ajali.
Makubaliano hayo mapya sasa yatazuia kusikilizwa kwa kesi ya Juni 23 ambayo kampuni hiyo ya kutengeneza ndege inakabiliwa na madai ya kuwapotosha waratibu Marekani kuhusu mfumo muhimu wa udhibiti wa safari za ndege kwenye 737 MAX, kuwa ndege aina hiyo inauzwa zaidi.