Wagonjwa wa saratani nchini Kenya watapata afueni baada ya malipo ya matibabu ya saratani kupungua.
Serikali inasema kuwa vipindi vya matibabu sasa vitagharimu dola 309 ( shilingi 40,000) badala ya bei ya sasa ya zaidi ya dola 900 ( shilingi 120,000).
Serikali imesema kupungua kwa gharama inatokana na ushirikiano kati ya Wizara ya Afya na kampuni ya matibabu ya Roche East Africa.
“Ushirikiano huu unalenga kuimarisha ulinzi wa kifedha kwa wagonjwa wanaopambana na saratani, mojawapo ya magonjwa yasiyoambukiza nchini Kenya (NCDs), kulingana na ajenda ya nchi ya Huduma ya Afya kwa Wote (UHC),” Waziri wa Afya Aden Duale amesema.
Roche ni kampuni kubwa zaidi ya kibayoteki duniani, yenye dawa zinazotofautishwa katika matibabu ya saratani, kinga ya mwili, na magonjwa ya kuambukiza.
"Ushirikiano huu sio tu kuhusu kupunguza gharama za matibabu unahusu pia kuokoa maisha, kukuza usawa, na kuimarisha uadilifu wa mfumo wetu wa huduma za afya," Duale aliongezea.
Chini ya makubaliano hayo, gharama ya kila kipindi cha matibabu imefikia dola 300 (shilingi 40,000), bila malipo ya pamoja yanayohitajika kutoka kwa wagonjwa.
Ushirikiano huo utatekelezwa katika vituo vyote vilivyo na kandarasi ya mfumo mpya wa biya ya afya maarufu kama SHA—ikiwa ni pamoja na hospitali za umma, za kidini na binafsi—kuhakikisha upatikanaji sawa wa huduma.
Serikali inasema chini ya ushirikiano huo, huduma zikakazoimarishwa ni pamoja na upatikanaji wa dawa muhimu za saratani na uchunguzi, uwezo na mafunzo kwa wahudumu wa afya katika udhibiti wa saratani ya matiti na mlango wa kizazi.
Pia kutakuwa na juhudi zaidi za uchunguzi na utambuzi wa mapema ili kusaidia uingiliaji kati kwa wakati.