Zaidi ya watu 170 wamekufa kwa ugonjwa wa kipindupindu nchini Sudan iliyokumbwa na vita ndani ya wiki moja, Wizara ya Afya imesema Jumanne.
Taarifa ya Wizara imesema kuwa watu 2,700 walipata ugonjwa huo ndani ya wiki moja tu, kati yao 172 walikufa.
“Vitengo 13 vya matibabu ya kipindupindu kwa sasa vinafanya kazi katika eneo la Khartoum, na MSF inasaidia vitengo saba kati ya hivyo ili kuhakikisha vinafanya kazi kikamilifu na vinaweza kuongezeka kulingana na mahitaji,” Shirika la MSF ambalo lina madaktari limesema katika akauti yake ya X.
Wizara hiyo ilisema asilimia 90 ya maambukizi ya kipindupindu yalirekodiwa katika Jimbo la Khartoum, ambapo nishati na usambazaji wa maji ulitatizwa katika wiki za hivi karibuni huku kukiwa na mapigano kati ya jeshi na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF).
Kulingana na takwimu za hivi punde zilizotolewa na Wizara hiyo, jumla ya wagonjwa wa kipindupindu nchini Sudan walifikia 60,993, na vifo 1,632.
“Mnamo Mei 21 pekee, kulikuwa na takriban wagonjwa 500 katika maeneo tofauti katika jimbo lote, ambao wanawakilisha robo moja ya kesi 2,000 zilizorekodiwa katika wiki tatu zilizopita na Wizara ya Afya mnamo 20 Mei,” Shirika la MSF limeongezea.
Mnamo Agosti 2024, mamlaka ya Sudan ilitangaza kipindupindu kuwa janga la kitaifa.
Hivi karibuni, jeshi la Sudan limepata tena udhibiti wa maeneo mengi katika Jimbo la Khartoum, ambalo linajumuisha miji mitatu ya mji mkuu - Khartoum, Bahri, na Omdurman - pamoja na eneo la Nile Mashariki.
Katika majimbo mengine 17 ya Sudan, RSF sasa inadhibiti sehemu tu za Kordofan Kaskazini na Magharibi na mifuko katika majimbo ya Kordofan Kusini na Blue Nile, pamoja na majimbo manne kati ya matano katika eneo la Darfur.
Tangu Aprili 2023, RSF imekuwa ikipambana na jeshi kwa ajili ya udhibiti wa Sudan, na kusababisha maelfu ya vifo na kusababisha moja ya migogoro mbaya zaidi ya kibinadamu duniani.
Zaidi ya watu 20,000 wameuawa na milioni 15 wamekimbia makazi yao, kulingana na Umoja wa Mataifa na mamlaka za mitaa.
Utafiti kutoka kwa wasomi wa Amerika, hata hivyo, unaweka idadi ya vifo kuwa karibu 130,000.