AFRIKA
2 dk kusoma
Shirika la WFP kupunguza msaada kwa watu Ethiopia
WFP inaonya kwamba kuendelea kuwepo kwa upungufu wa fedha kunatatiza uwezo wake wa kuendeleza utoaji wa misaada ya chakula nchini Ethiopia kwa watu waliolazimika kuhama makazi yao na wakimbizi.
Shirika la WFP kupunguza msaada kwa watu Ethiopia
WFP inatoa usaidizi kwa maeneo ya Afar na Oromia yaliyoathiriwa na mitetemeko ya ardhi na kulazimisha watu kuhama makwao / Picha: WFP Ethiopia / Public domain
30 Mei 2025

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) linasema litalazimika kupunguza misaada inayotoa kwa watu nchini Ethiopia kwani "linatarajia kusitishwa kwa ufadhili mwezi Juni 2025."

WFP inaonya kwamba upungufu wa fedha unaoendelea unazuia uwezo wake wa kuendeleza msaada wa chakula nchini Ethiopia kwa walilazimika kuhama makazi yao pamoja na wakimbizi.

Katika ripoti yake ya mwezi Aprili, WFP ilisema "ililazimika kupunguza kiwango cha chakula inachogawa hadi asilimia 65 ya mgao wa kawaida kutoka asilimia 80 mwezi Februari.".

Mgao wa sasa unajumuisha kilo 9 za nafaka, kilo 1 ya kunde na kilo 1.1 ya mafuta kwa kila mtu kwa mwezi.

Hili pia litaathiri wakimbizi wanaoishi nchini Ethiopia.

WFP ilisema hii "itapunguza kwa kiwango kikubwa mgao kutoka asilimia 60 ya kifurushi cha kawaida cha chakula mwezi Aprili hadi asilimia 50 mwezi Mei" kutokana na vikwazo vya ufadhili.

"Ethiopia inaendelea kukumbwa na migogoro, ukame, mafuriko, na mfumuko wa bei, na hivyo kuzidisha uhaba wa chakula," WFP ilisema.

Katika ripoti yake ya Aprili WFP inasema iliweza kuwafikia watu 881,430 Wakimbizi wa Ndani (IDP) katika mikoa ya Afar, Somali na Tigray. Hii ni takriban asilimia 93 ya waliokuwa wanalengwa.

“WFP pia ilifikia wakimbizi 797,370 katika kambi na maeneo 29 na hapo kufikia asilimia 92 ya lengo lake la kila mwezi. Hata hivyo, tulifikia asilimia 41 pekee ya watu waliotakiwa kupata msaada katika kambi za wakimbizi kwa msaada wa lishe ya afya zaidi kutokana na uhaba wa chakula cha aina hiyo nchini," WFP imesema.

"Wakati makubaliano ya amani yalimaliza mzozo uliokithiri katika eneo la Kaskazini la Tigray, mapigano ya silaha katika maeneo mengine, hasa katika Amhara na Oromia, yaliongeza matatizo, na hii imetatiza shughuli za WFP, na kuifanya kuwa changamoto zaidi kuwafikihsia watu chakula kwa njia salama na kwa wakati kwa wakazi walio hatarini zaidi, " shirika hilo limeongeza.

Hapo WFP ilitangaza kusimamisha mradi wake wa lishe kwa wanawake na watoto 650,000 wenye utapiamlo kuanzia mwezi Mei, wakitaja sababu kuwa upungufu mkubwa wa fedha.

Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us