Serikali ya Kenya imeamua kununua mchele wote unaozalishwa na wakulima wa mchele wa eneo la Mwea, katika kaunti ya Kirinyaga, katikati mwa nchi.
Wizara ya kilimo imesema serikali itanunua tani 5000 za mchele kwa wakulima hao ambao wamelalamika kukwama na mazao yao kufuatia ununuzi wa mchele kutoka nje ya nchi .
“Ili kuhakikisha wakulima zaidi ya 8500 kutoka Kirinyaga wanapata riziki pamoja na wale wa kaunti jirani, Kampuni ya Kenya National Trading Corporation (KNTC) itanunua zaidi ya tani 5000 za mchele unaokuzwa nchini wenye thamani ya zaidi ya dola milioni 3.8 (shilingi milioni 500 ).
Uamuzi huu unafuatia wito wa wakulima kwa serikali kusimamisha kwa muda ununuzi wa mchele kutoka nje ya nchi, ili waweze kuuza mavuno yao.
Wakulima hao wanazalisha chini ya mradi wa kilimo cha umwagiliaji wa Mwea.
Hili ni eneo la kubwa zaidi la kilimo cha umwagiliaji nchini Kenya lenye historia ya takriban miaka 60. Mpango huu umechangia ukuaji wa sekta ya mpunga nchini Kenya huku ugavi wa zaidi ya 60% ya mchele wa nchini Kenya ukitoka Mwea.
“ Chama cha ushirika wa wakulima kitapokea malipo kamili mwezi mmoja baada ya mchele wote kununuliwa. Huu ni mfumo bora wa malipo tofauti na hapo awali ambapo ulitatiza shughuli za wakulima na upatikanaji wa pesa.” Dkt. Bruno Linyiru , Mkurugenzi Mkuu wa Kilimo na Chakula alisema.
Wizara ya kilimo inasema Kenya ilizalisha tani 191,000 za mchele mwaka 2024/2025.
“Hii inaweza kutumika kwa miezi miwili tu kwa sababau mahitaji ya mchele nchini kwa mwezi ni takriban tani laki moja,” Dkt. Linyiru ameongeza.
Amesisitiza kuwa tangu Januari 2025, ni tani 94,000 pekee za mchele zimenunuliwa kutoka nje ya nchi.
Upungufu huu hivyo unalazimu ununuzi wa mchele kutoka nje ya nchi ili kuhakikisha kuongezeka kwa usambazaji wa ndani wa nafaka hii ambayo ni ya tatu kwa kuliwa zaidi baada ya mahindi na ngano.