AFRIKA
5 DK KUSOMA
Adela na Adelina, mapacha walioanza kutetea haki za watoto wakiwa wadogo
Mabinti wawili, Adela Alex na Adelina Alex ambao ni mapacha waliopo jijini Dar es Salaam nchini Tanzania, ni miongoni mwa mabinti wachache nchini humo walioanza kujiingiza katika harakati za kutetea haki za watoto wenzao wakiwa na umri mdogo kabisa.
Adela na Adelina, mapacha walioanza kutetea haki za watoto wakiwa wadogo
Adela na Adelina, mabinti mapacha kutoka Dar es Salaam, Tanzania. Picha/TRT Afrika.  / Others
1 Januari 2024

Na Mwandishi wetu

TRT Afrika, Dar es Salaam, Tanzania

Adela Alex na Adelina Alex ni mabinti wawili ambao nyuso zao siku zote zimejawa na furaha. Tabasamu pana ndilo linalopamba nyuso zao. Kama majina yao yanavyofanana, ndivyo sura zao zinavyofanana hivyo hivyo.

Hawa ni mabinti mapacha, waliopo jijini Dar es Salaam nchini Tanzania. Wana umri wa miaka 13, wakijiandaa kuanza kidato cha kwanza wakati wowote kuanzia sasa.

Hata hivyo, ni miongoni mwa mabinti wachache nchini humo ambao wameonyesha ujasiri wa kuanza kutetea haki za watoto wenzao wakiwa na umri mdogo kabisa.

Chanzo cha harakati zao

Harakati zao zimejikita zaidi, hasa katika kutetea haki za watoto hasa wale wanaonyanyapaliwa kutokana na sababu mbalimbali.

Msukumo wa harakati zao ulianzia mwaka 2016 baada ya Adela kuanza kunyanyapaliwa shuleni na hata kwenye jamii yake kutokana na tatizo la mfumo wa hewa.

"Adela anasumbuliwa na tatizo la mfumo wa hewa ambao unasababisha mawimbi yake ya ubongo kucheza na mpaka sasa haujagundulika jina lake. Ndio maana tuko katika utafiti kwa sababu hata dawa anazotumia, sio zinazotibu huo ugonjwa," anasema Sara Emmanuel Kitainda, ambae ni mama mzazi wa watoto hao.

Adela alimwambia mwandishi wa TRT Afrika, kuwa hali hiyo imemfanya kubandikwa majina ambayo hayapendi hasa akiwa shule, na wakati mwengine, kulinganishwa na Adelina kwenye matokeo ya mitihani.

“Katika suala la ufaulu wa masomo, mara nyingi nalinganishwa na mwenzangu ambae anafaulu kuniliko. Wananiambia kwamba mwenzangu ana akili kuniliko kwa sababu mimi nacheza darasani,” anasema Adela.

Kwa sasa mabinti hawa, chini ya usaidizi wa mama yao, wako katika hatua za mwisho za kusajili taasisi yao itakayoitwa ‘Adela Foundation’ lengo lake ni kuongeza nguvu katika harakati zao.

"Mara nyingi jamii inawaona watoto kama hawajui haki zao, hivyo jukumu la kuwalinda huachiwa wazazi na walezi. Lakini mambo yamebadilika hivi sasa, matumizi ya mitandao na teknolojia inawajengea watoto uelewa wa kutambua haki zao mapema zaidi," anasema Sara.

Wamekuwa wakizunguka mashuleni, na kuandaa makongamano mbalimbali ili kufikisha elimu ya kuupinga ukatili kwa watoto na ukiukwaji wa haki za binadamu kwa ujumla.

Tangu walipoanza harakati hizo licha ya kuwa na matokeo chanya katika baadhi ya maeneo, lakini wamekuwa wakikabiliwa na changamoto hasa kutokana na kasumba iliyoko ndani ya jamii kwamba watoto hawawezi kuwakosoa wakubwa.

Adelina anasema mara kadhaa wamekuwa wakionekana kama hawana adabu kutokana kuendesha harakati hizo za kudai haki na maslahi ya watoto.

“Ukiwa mwanaharakati ukisema hiki sio kizuri unaonekana huna adabu,” anasema Adelina.

Kutokana na kasumba hii wamekuwa wakinyimwa nafasi ya kuzungumza kwenye majukwaa mbalimbali na wakati mwingine kwenye yale machache wanayopatiwa nafasi wameishia kuzomewa kwamba wanapoteza muda.

Shule na uana harakati

Lakini swali linaloweza kuibuka ni je, mabinti hawa wanawezaje kugawa muda wao katika masomo na shughuli zao za kutetea haki za watoto?

Mama yao anasema kuwa, kutokana na shughuli zao kugusa jamii, na maisha ya kila siku, hivyo wakiwa shule, hasa wakati wa mapumziko, wao huendelea kutoa elimu kwa wenzao.

"Wanapofunga shule, ndio wanakuwa majukwaani au kwenye vyombo vya habari na matamasha mbalimbali," anasema.

Ndoto yao

Hata hivyo, mbali na harakati zao, bado watoto hawa wana ndoto ya kufika mbali zaidi katika masomo yao. Adela asema yeye ndoto yake ni kuwa mwanasheria, huku Adelina nae, akitamani kuwa mhandisi wa ndege.

CHANZO:TRT Afrika
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us