Utajiri wa Afrika: Wafahamu Sili wa kahawia kutoka Afrika Kusini
Utajiri wa Afrika: Wafahamu Sili wa kahawia kutoka Afrika Kusini
Kando ya pwani ya Namibia na pwani ya Magharibi na Kusini mwa Afrika Kusini, ndiko wanapopatikana sili wa kipekee, wenye manyoya ya kahawia.
30 Mei 2025

Ukitembelea pwani ya Afrika Kusini utakutana na mnyama anayeitwa Sili, au ‘Seal’, kwa lugha ya kiingereza. 

Huyu ni mnyama anayeishi ardhini na majini.

Kando ya pwani ya Namibia na pwani ya Magharibi na Kusini mwa Afrika Kusini, ndiko wanapopatikana sili wa kipekee, wenye manyoya ya kahawia.

Katika eneo hilo, wanapatikana sili takriban milioni mbili, wengi wao wakiishi katika vikundi vya sili 25 hadi 40 kwenye miamba ya pwani na visiwani.

Mnyama huyu ana uwezo kubeba ujauzito kwa kipindi cha miezi tisa hadi kumi na moja. 

Wanyama hawa huzaliwa kati ya miezi ya Novemba na Disemba na maisha huanzia ardhini, chini ya uangalizi wa mama zao.

Wanapozaliwa, huwa na rangi nyeusi, baadaye hubadilika na kuwa kijivu wanaponyauka katika miezi michache ya kwanza ya maisha yao. Baada ya muda manyoya yanapata rangi ya kahawia.

Kwa kipindi cha miezi sita, hunyonyeshwa na mama zao. Kwa sababu watoto hawazaliwi na mafuta ya kuhami joto, hivyo hawaingii majini mpaka baadae kidogo.

Sili jike hufikia ukomavu wakiwa na umri wa miaka mitatu au minne, na dume wakiwa na miaka minne au mitano.

Lakini kwa kawaida, huzaa tu wakiwa na umri wa takriban miaka 10. Kwa ujumla, sili anaweza kuishi hadi miaka 21.Sili wa kiume huwa wazito zaidi, wanaweza kufikia kilo 350, huku wa kike anafikia kilo 150.

Wakiwa katika vikundi vyao hutafuta samaki na wakati mwingine ngisi, wakiwa na uwezo wa kupiga mbizi hadi kina cha mita 200.

Wakiwa ardhini sili wa manyoya hulala kama sisi wanadamu, na ni wapandaji wenye ujuzi, wanaweza kuonekana katika sehemu za juu ajabu.

Lakini ndani ya maji wana uwezo wa kufunga sehemu tofauti za ubongo wao kwa nyakati tofauti ili kupumzika huku wakiendelea kubaki katika vikundi vyao.

Baharini wanajulikana kwa uwezo wao wa kusafiri umbali mkubwa - kama vile kilomita 80 kwa siku.

Nchini Afrika Kusini, sili wamekuwa spishi inayolindwa, uwindaji wake ulipigwa marufuku 1990.

Hata hivyo nchini Namibia, ambapo kuna asilimia 75 ya sili wa manyoya, uwindaji si haramu , msimu wa uwindaji wa kila mwaka hufanyika kati ya Agosti na Novemba.


Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us