Uraibu uliofichwa kwa peremende: Mapambano ya Afrika kuzuia vijana dhidi ya nikotini yenye ladha
AFRIKA
4 dk kusoma
Uraibu uliofichwa kwa peremende: Mapambano ya Afrika kuzuia vijana dhidi ya nikotini yenye ladhaAfrika inakabiliana na vita dhidi ya bidhaa za tumbaku zenye ladha ambazo huongeza uraibu miongoni mwa vijana wakiona kama starehe isiyo na madhara.
Wanafunzi wengi wameripotiwa kutumia pesa zao za mlo kununua nikotini yenye ladha badala ya chakula. / Reuters
12 Juni 2025

Mikono ya Adeola* ilitetemeka tena. Si kwa sababu ya hofu au baridi, bali ni ishara ya kuwa na hamu ambayo sasa ilionekana kutawala maisha yake.

Kulegeza kamba kwa hamu hiyo kulimaanisha kutumia pesa za matumizi kununua nikotini badala ya chakula. Kibaya zaidi ilikuwa kujua kwamba afueni hiyo ingekuwa ya muda mfupi tu.

Msichana huyo wa miaka 17 kutoka Nigeria hakudhania kuwa maisha yake yangechukuwa mwelekeo huu alipokuwa akijaribu ‘sigara ya kielektroniki’ au ‘vape’ yenye ladha ya stroberi miezi kadhaa iliyopita.

"Ilikuwa na ladha kama peremende au pipi," Adeola anaiambia TRT Afrika. "Marafiki zangu walisema hata si kama kuvuta sigara halisi... Sikutegemea kwamba ingeniathiri hivi."

Swali linalowakabili baadhi ya vijana wa Afrika si kama watakutana na bidhaa za nikotini zenye ladha ya kuvutia – bali ni muda gani kabla ya ladha za stroberi, pipi kuwasha, na pamba yenye utamu kufichua madhara yao halisi.

Nchini Kenya, Jamal* mwenye umri wa miaka 16 anakabiliana na changamoto za uraibu wa kuvuta vape na dalili za kuacha nikotini, hali inayofanana na ya Adeola.

Alianza kutumia nikotini zenye ladha ya pipi kuwasha akiwa na miaka 14, akivutiwa na ladha ya minti na imani kwamba zilikuwa hazina madhara zaidi kuliko sigara.

"Mwanzoni ilikuwa tu kwa ajili ya kujifurahisha. Kisha nikashindwa kuacha," anakiri kijana huyo wa Nairobi. "Nilikuwa napata maumivu ya kichwa na kuhisi mgonjwa nikizikosa."

Lakini Jamal alipambana. Kwa msaada wa kikundi cha vijana cha kupinga tumbaku, aliacha baada ya miezi sita kwa kupitia changamoto.

"Kuachana na uraibu huo ilikuwa jambo gumu zaidi nililowahi kufanya," anaieleza TRT Afrika. "Sasa, nawaonya marafiki zangu: ladha hizi ni mtego."

Janga linalokua

Katika Siku ya Dunia ya Kutovuta Tumbaku 2025, inayoadhimishwa Mei 31, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitoa wito wa dharura kwa serikali kote ulimwenguni kupiga marufuku bidhaa zote za tumbaku na nikotini zenye ladha ili kuwalinda vijana dhidi ya janga linaloendelea kukuwa.

"Ladha zinachochea wimbi jipya la uraibu na zinatakiwa kupigwa marufuku," anasema Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus. "Zinaharibu miongo ya maendeleo katika udhibiti wa tumbaku."

Zaidi ya nchi 50 zimepiga marufuku tumbaku zenye ladha, huku zaidi ya 40 zikizuia uuzaji wa sigara za kielektroniki. Lakini vifaa vya nikotini kama vichujio vya vidonge na matone ya ladha yanayopenyezwa bado hayajadhibitiwa kikamilifu.

Hata hivyo, baadhi ya mataifa ya Afrika yanachukuwa hatua. Afrika Kusini, Mauritius na Ethiopia zimeweka vikwazo kwa sigara za kielektroniki na tumbaku zenye ladha, huku Kenya ikifikiria kanuni kali zaidi baada ya ripoti za watoto wa shule kutumia nikotini.

Hata hivyo, utekelezaji unakabiliwa na changamoto, kwani sekta ya tumbaku inatumia watu mashuhuri katika mitandao ya kijamii, vifungashio vya kuvutia, na ladha mbalimbali kuwavutia watumiaji vijana.

Dkt. Rüdiger Krech, Mkurugenzi wa WHO wa idra ya uimarishaji afya, kuficha maneno yake kuhusu mbinu za ufungashaji na uuzaji katika sekta ya nikotini.

"Tunashuhudia kizazi kikitekwa na nikotini kupitia pakiti zenye ladha ya ubani na ‘vape’ za rangi za upinde wa mvua," anasema. "Huu si ubunifu, ni udanganyifu. Na tunatakiwa kuupiga vita."

Mtego wa ladha

Wataalamu wa matibabu wanaunga mkono wasiwasi wa WHO kuhusu mwenendo unaokuwa wa kuonyesha kuvuta ‘vape’ kama jambo lisilo na madhara makubwa ikilinganishwa na sigara za kawaida.

Dkt. Asha Mohamed, mtaalamu wa magonjwa ya mapafu huko Nairobi, anasema kwa wasiwasi juu ya idadi inayoongezeka ya watu wanaopambana na magonjwa yanayosababishwa na kuvuta ‘vape’.

"Wagonjwa vijana wanakuja wakiwa na muwasho mkali wa mapafu, bila kutambua kwamba ladha hizi ‘za kufurahisha’ wanazozitegemea zinapeleka kemikali zenye sumu moja kwa moja ndani ya miili yao," anaiambia TRT Afrika.

Licha ya serikali na wanaharakati kupambana dhidi ya mbinu za sekta hiyo, vifo milioni nane vinavyohusiana na tumbaku kila mwaka vinaonyesha kuwa bado safari ni ndefu.

Kwa Adeola na Jamal, vita ni vya kibinafsi. Wamepitia hatari za uraibu wa nikotini na wamefanikiwa kwa sababu ya nia yao ya kuacha.

Baada ya miezi ya mapambano, Adeola aliacha kutumia bidhaa za nikotini zenye ladha. Anawahofia wenzake wa rika lake ambao hawajaweza kufanya hivyo.

"Hawajui jinsi ladha hizi zilivyo hatari," anasema.

Jamal anakubaliana kabisa. "Usidanganywe na ladha," anasema. "Ladha ni tamu, lakini uraibu ni mchungu," alisisitiza kwa TRT Afrika.

*Majina mengine yamebadilishwa ili kulinda utambulisho wao.

CHANZO:TRT Afrika
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us