Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis ameendelea kupokea matibabu hospitalini Gemelli jijini Roma, akisumbuliwa na maradhi ya homa ya mapafu.
Hata hivyo, siku ya Jumanne Vatican ilisema kuwa kiongozi huyo mwenye umri wake 88 hakuhitaji msaada wa oksijeni wakati wa kulala.
Kulingana na madaktari wa hospitali ya Gemelli, afya ya Papa Francis inaendelea kuimarika baada ya kupata shida ya kupumua, hali iliyoibua hofu kuhusu afya yake.
Hata hivyo, madaktari hao hawakuwa tayari kusema ni lini Papa Francis ataruhusiwa kutoka hospitali.
"Afya yake imezidi kuimarika, ukizingatia kuwa hakuhitaji msaada wa oksijeni,” Vatican ilisema.
Hata hivyo, Vatican ilisisitiza kuwa kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani ataendelea kutumia mipira maalumu yenye kuingizwa kwenye pua zake, ili kumsaidia kupumua.
Papa Francis, ambaye aliondolewa pafu moja akiwa kijana, ana historia ya kusumbuliwa na maradhi ya kupumua.