Hatua ya pili ya mazungumzo ya amani ya Urusi na Ukraine imekamilika katika Ikulu ya Istanbul ya Ciragan siku ya Jumatatu baada ya zaidi ya saa moja, mwandishi wa Anadolu ameripoti.
Urusi iliwakilishwa na ujumbe ulioongozwa na msaidizi wa rais Vladimir Medinsky, huku ujumbe wa Ukraine ukiongozwa na Waziri wa Ulinzi Rustem Umerov.
Ujumbe wa Ukraine pia ulijumuisha waziri wa mambo ya nje, mkuu wa idara ya ujasusi, na mkuu wa majeshi.
Akizungumza na waandishi wa habari katika kongamano la Vilnius, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy alithibitisha kumalizika kwa mazungumzo hayo, akisema kuwa anasubiri taarifa za Umerov.
"Walibadilishana (wajumbe) nyaraka kupitia wawakilishi wa Uturuki, na tunajiandaa kuwaachilia huru wafungwa wa vita," alisema.
Kufuatia mazungumzo hayo, Andriy Yermak, mkuu wa ofisi ya rais wa Ukraine ambaye pia ni mjumbe, alisema kwenye mtandao wa Telegram kuwa Ukraine ilisisitiza kuhusu kurejeshwa kwa watoto, ambao, kulingana na Ukraine "walihamishwa kinyume na sheria,kulazimishwa kuondolewa" hadi kwenye maeneo yanayodhibitiwa na Urusi.
Jiji la Istanbul pia lilikuwa mwenyeji wa hatua iliyotangulia 16 Mei, ambayo matokeo yake yakawa kubadilishana idadi kubwa ya wafungwa kati ya mataifa hayo mawili tangu kuanza kwa mapigano ya Urusi na Ukraine, ambayo sasa yako mwaka wake wa nne.
Uturuki imeendeleza ushirikiano wa karibu na nchi zote Urusi na Ukraine kipindi chote cha vita na muda wote imekuwa iko tayari kuratibu upatanishi wa juhudi za majadiliano na amani.