Waokoaji walipata miili zaidi siku ya Jumamosi kutokana na mafuriko yaliyokumba mkoa wa Eastern Cape wa Afrika Kusini mapema wiki hii, huku idadi ya waliofariki ikifika 86.
Rais Cyril Ramaphosa alitembelea mkoa huo siku ya Ijumaa na kusema kuwa "janga hilo baya" lilitokana na mabadiliko ya tabianchi.
Waziri wa Polisi Senzo Mchunu alisema Jumamosi kuwa amepokea taarifa za "idadi ya waliofariki kutoka mkoa huo imefika 86".
Ramaphosa alikadiria kuwa mafuriko yalifika urefu wa mita nne baada ya mvua kubwa na upepo mkali kuharibu Eastern Cape.
Nyumba zimezama
Maelfu ya nyumba, barabara, shule na vituo vya afya zilikuwa zimezana kwenye matope ya mafuriko.
Eneo lililokumbwa vibaya na mafuriko na maporomoko ilikuwa ni mji wa Mthatha, karibu kilomita 800 kusini mwa Johannesburg.
Waokoaji walienda nyumba hadi nyumba wakijaribu kutafutaa miili na kama kuna watu ambao wangeokolewa, baada ya watu kukwama katika nyumba zao.
Wengine walifanikiwa kukimbia kupitia paa za nyumba zao, ambapo walilazimika kusubiri kwa muda mrefu.
Miongoni mwa waliokufa ni watoto wasiopungua sita na watu wakubwa watatu waliokuwa ndani ya basi ambalo lilisombwa na mafuriko.
‘Hali mbaya ya hewa’
Wanafunzi watatu waliokolewa baada ya kung’ang’ania juu ya mti lakini wanne walikuwa bado hawajapatikana kufikia Jumamosi.
Theluji na mvua kubwa ni hali ya kawaida wakati wa msimu wa baridi kali nchini Afrika Kusini lakini maeneo ya pwani yalikumbwa na "hali mbaya ya hewa", Ramaphosa alisema siku ya Alhamisi.
Kulingana na shirika la Green Climate Fund, nchi hiyo inakabiliwa na athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi, ambayo inafanya kuwe na hali mbaya zaidi.