Iran imesema mazungumzo na Marekani kuhusu mpango wa nyuklia wa Tehran "hayana maana" baada ya shambulio kubwa zaidi la kijeshi la Israel dhidi ya adui yake wa muda mrefu, ikiishutumu Washington kuunga mkono shambulio hilo.
"Upande wa pili (Marekani) ulifanya kwa njia ambayo inafanya mazungumzo kutokuwa na maana. Huwezi kudai kujadili na wakati huo huo kugawanya kazi kwa kuruhusu utawala wa Kizayuni (Israel) kulenga eneo la Iran," Shirika la Habari la Tasnim lilimnukuu msemaji wa Wizara ya Mambo ya Mje Esmaeil Baghaei akisema Ijumaa.
Alisema Israel "ilifanikiwa kuathiri" mchakato wa kidiplomasia na shambulio la Israel lisingetokea bila ya idhini ya Washington.
Iran hapo awali iliishutumu Marekani kwa kuhusika na mashambulizi la Israel, lakini Washington ilikanusha madai hayo na kuiambia Tehran katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba itakuwa "busara" kujadiliana kuhusu mpango wake wa nyuklia.
Duru ya sita ya mazungumzo ya nyuklia kati ya Marekani na Iran ilipangwa kufanyika Jumapili mjini Muscat, lakini haijafahamika iwapo mazungumzo hayo yatafanyika baada ya mashambulizi ya Israel. Iran inakanusha kuwa mpango wake wa kurutubisha madini ya uranium ni kwa ajili ya shughuli za kiraia, ikikataa madai ya Israel kwamba inatengeneza silaha za nyuklia kwa siri.
Rais wa Marekani Donald Trump aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba yeye na timu yake walijua kwamba mashambulizi ya Israel yanakuja lakini bado wanaona nafasi ya kupata muafaka.