Ulikuwa huizungumzii Man U, bila kumtaja Babu Fergie kipindi hicho.Unajua alipo kwa sasa gwiji huyu mtafuna ‘Big G’ au ubani?
Hivi ni kweli Alex Ferguson ndiye aliyeondoka na nyota ya Manchester United kama Aslay alivyosepa na daftari la nyimbo pale Yamoto Band?
Sir Alex Ferguson alihudumu kama kocha wa Mashetani Wekundu pale Old Trafford kuanzia mwaka 1986 hadi 2013, na miaka 12 baada ya babu Fergie kuachana na soka, Man U hawajashinda taji lolote la Ligi Kuu ya England zaidi ya Kombe la FA ambalo walishinda mwaka 2016 na 2024, huku Kombe la EFL wakitwaa mara mbili, 2017 na 2023.
The Red Devils wakabeba Ngao ya Jamii mwaka 2016 kabla ya kutwaa taji la ligi ya Europa mwaka 2017.
Kwa ujumla Mancheseter United imeshinda mataji ya EPL mara 20 kati ya hizo mara 13 ilikuwa chini ya moja wa makocha bora zaidi katika soka.
Sir Alexander Chapman Ferguson alizaliwa mjini Glasgow, huko Scotland miaka 83 iliopita.
Wakati wa ujana wake, Babu Fergie alichezea vilabu mbalimbali nchini Scotland, ikiwemo Rangers, ambapo aliibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Uskochi kwenye msimu wa 1965-66.
Aliwahi kuchaguliwa kufundisha kwenye ligi hiyo na pia kufanikiwa kuipeleka timu ya taifa Kombe la Dunia mwaka 1986.
Katika kipindi chake cha miaka 26 alichokoongoza benchi la ufundi Old Trafford, Babu Fergie ameshinda jumla ya mataji 38, akiwa ndiye meneja aliyehudumu muda mrefu zaidi katika timu hiyo.
Tangu kuondoka kwake, Man U imefundishwa na mameneja wanane, katika kipindi cha miaka 12, huku wengi wakidema dema na kuhatarisha Man U ishuke daraja.
Kwa sasa, Man U sio Mashetani Wekundu tena, bali ni kichwa cha mwendawazimu. Je, ni kweli kuondoka kwa Babu Fergie ndio chanzo cha mkosi wa Man United?