Wengi huwa wanajiuliza Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ingekuwaje hii leo kama Patrice Lumumba asingeuwawa?
Ama kwa hakika, kijana huyo wa miaka 35 alikuwa na ndoto kubwa ya kuiona nchi yake ikiwa ya amani na maendeleo.
Waandishi wengi wa vitabu, akiwemo Raoul Peck na Yves Pinguilly, wamemsifu Patrice Lumumba kwa mchango wake katika mapambano ya kuikomboa nchi yake.
Usuli wake
Akifahamika zaidi kwa mtindo wake wa nywele, kama ilivyokuwa kwa kofia ya Ernesto Che Guevara, Lumumba alizaliwa katika eneo la Onalua, ambalo kwa sasa linaitwa Sankuru.
Baada ya kupata elimu kutoka shule za misheni za Wakatoliki na Waprotestanti, alionesha kupenda zaidi masomo ya sayansi.
Hata hivyo, hapo baadae Patrice Lumumba alijikuta akifanya kazi ya uandishi wa habari jijini Kinshasa.
Akiwa na miaka 29, Patrice Lumumba, wakati huo akifa mfanyakazi wa posta katika eneo la Kisangani, alianza kuandikia magazeti, hasa nyakati za mapambano ya kudai uhuru.
Kuingia kwenye siasa
Mwaka 1955, Patrice Lumumba aliasisi chama cha APIC, kabla ya kujiunga na chama cha Liberal kilichokuwa na maofisa kutoka Congo na Ubelgiji.
Mwaka huo huo, Patrice Lumumba alitupwa jela baada ya kutuhumiwa na kujihusisha na ubadhirifu fedha za posta.
Hata hivyo, aliendelea na mapambano yake muda mfupi baada ya kutoka jela, akishinikiza mazingira mazuri na malipo mazuri kwa wafanyakazi.
Miaka mitatu baadaye, akiwa pamoja na Gaston Diomi Ndongala na Joseph Ileo, alianzisha chama cha National Movement, ambacho kilijipatia umaarufu mkubwa kwa wakati huo.
Disemba mwaka huo, Patrice Lumumba alikutana na mwanamapinduzi kutoka Ghana, Kwame Nkrumah, ambaye alikuwa ameanzisha vuguvugu la uhuru barani Afrika.
Akiwa anahutubia umati wa watu 10,000 nchini kwake, Patrice Lumumba aliweka wazi vipamumbele vya chama cha MNC, vyenye kulenga kukomesha ukoloni.
Vuguvugu hilo lilipiga marufuku mikutano ya chama cha ABAKO na kusababisha vifo vya watu 42, na kufurushwa kwa kiongozi wa kwanza wa nchi hiyo Joseph Kasa-Vubu, aliyekimbilia Ubelgiji.
Muda mfupi baadaye, baada ya mkutano mkuu wa MNC, wanajeshi waliwashambulia kwa risasi umati wa watu katika jiji la Kisangani, na kuua watu wapatao 30, huku Lumumba akikamtwa na kuhukumiwa kifungo cha miezi sita jela mwezi Januari 1960.
Hata hivyo, jina la Lumumba likazidi kujipatia umaarufu, na hivyo kupelekea shinikizo la kumwachia Patrice Lumumba kutoka kifungoni.
Hatua hiyo ilipelekea mgogoro kati ya serikali ya Ubelgiji na chama cha United Front.
Siku ya Uhuru
Ni viongozi wawili tu ambao walioruhusiwa kuzungumza siku ya uhuru Juni 30, 1960.
Viongozi hao ni Mfalme Baudouin wa Ubelgiji na Rais Kasa-Vubu.
Katika risala yake, mfalme huyo alisema kuwa nchi yake iliamua kuizawadia Congo uhuru, kauli ambayo haikupingwa na rais wa nchi hiyo.
Kwa upande wake, Lumumba alipanda jukwaani kutoa hotuba yake.
''Kama itakubaliwa hii leo kwa makubaliano na Ubelgiji, hakuna raia yoyote wa Congo atakayekuja kusahau namna nchi yetu ilivyonyakuliwa.
Yalikuwa ni machozi, jasho na damu, tukipambana dhidi ya udhalimu wa kikoloni.
Bado tunakumbuka mateso, dhihaka, matusi na kejeli tulizopewa kutokana na rangi ya ngozi yetu.
Tulijua namna ardhi yetu ilivyoporwa.
Tunajua kuwa sheria haikuwa sawa, ikitegemea kama itamhusu mtu mweupe au mweusi.
Nani atasahau mauaji ya ndugu zetu mitaani?
Kwa sasa, nchi yetu iko mikononi mwetu […] ''.
Katika risala zao, viongozi wa kisiasa nchini humo waliangazia amani ya nchi, maendeleo ya kiuchumi na usawa kati ya bara la Afrika na mataifa ya magharibi.
Hatma yake
Licha ya risala yake kukubalika na watu wengi wakiwemo vijana, wako walioipokea tofauti.
Muda si mrefu, baadhi ya Wakongomani wakaanza kulumbana na maofisa wa Kibelgiji na kupelekea kuuwawa kwa baadhi ya maofisa hao.
Machafuko hayo yaliendelea kushika kasi na kusambaa nchi nzima.
Huku kukiwa na shinikizo kutoka jumuiya za kimataifa ikiwemo Marekani mnamo Septemba 4, 1960, Rais Joseph Kasa-Vubu alitangaza kwa njia ya redio kufukuzwa kazi kwa Lumumba.
Hatua hiyo ilipingwa na Lumumba akimtuhumu Rais Kasa-Vubu kwa uhaini.
Muda mfupi baadae, Joseph Désiré Mobutu alitwaa madaraka ya nchi kwa njia ya mapinduzi.
Mnamo Oktoba 10, 1960, Mobutu alimuweka Lumumba kizuizini.
Mwezi mmoja baadae, Lumumba, akiwa na familia yake alitoroka kutoka eneo alilokuwa akiishi la Kalina na kuelekea jijini Kinshasa, kabla ya kukamatwa Disemba 1 katika wilaya ya Sankuru.
Ilipofika Januari 17, 1961 Patrice Lumumba na wenzake wawili Maurice Mpolo na Joseph Okito, walikabidhiwa kwa mamlaka za Katanga, na kuanza kuteswa.
Waliuwawa kwa kupigwa risasi jioni hiyo hiyo kufuatia amri iliyotolewa na afisa wa Kibelgiji.
Nyaraka na simulizi mbalimbali zinaonesha kuwa mwili wa Lumumba uliyeyushwa kwenye tindi kali ili kupoteza ushahidi wa mauaji yake.
Mwaka 2016, mahakama za Ubelgiji zilichukua jino la shujaa huyo, na miaka sita baadaye, kuamua kukabidhi kwa mamlaka za DRC.
Kwa sasa, jino hilo limehifadhiwa na familia ya Patrice Lumumba.