Na Susan Mwongoli
Kati ya almasi 20 kubwa zaidi kuwahi kugunduliwa, nne zilitoka katika ardhi ya Sierra Leone.
Kwa kushangaza, licha ya kuwa juu ya hazina kubwa ya almasi, dhahabu, maadini ya ‘rutile’, jiwe la ‘bauxite’ ambayo ni maadini asili yanayotowa alumini, maadini ya chuma na madini mengine, taifa hili la Afrika Magharibi linasalia kuwa miongoni mwa mataifa maskini zaidi duniani - ikisalia kuwa mfano wa nchi zenye laana ya rasilimali.
Sasa, zaidi ya miongo miwili tangu kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyosambaratisha nchi hiyo, Sierra Leone inaanzisha kampeni kabambe ya kubadilisha utajiri wake wa madini kuwa chanzo endelevu cha ustawi wa kiuchumi kwa wakazi wake.
Sura ya hivi punde zaidi katika juhudi hii ilifunuliwa mjini Istanbul mwishoni mwa Mei, ambapo serikali ya Sierra Leone iliandaa mkutano wa biashara na uwekezaji ili kuvutia wawekezaji wa kimataifa, hasa kutoka Uturuki.
Wawekezaji kutoka sehemu nyingine za Ulaya, Afrika na Asia, wakiwemo wengi ambao tayari wanafanya biashara nchini Sierra Leone, pia walihudhuria.
"Sierra Leone ni demokrasia inayofanya kazi kikamilifu, ambayo inafanya nchi yetu kuwa na mazingira ya kulinda uwekezaji," balozi wa nchi hiyo nchini Utruki, Timothy Musa Kabba, aliwaambia waliohudhuria.
Semina ya Mei 30, iliyoandaliwa na Ubalozi wa Sierra Leone huko Ankara, iliwakilisha zaidi ya uhamasishaji wa kidiplomasia; ilionyesha juhudi za Sierra Leone kuandika upya simulizi ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikifafanuliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe, magonjwa na umaskini.
Waandalizi wa kongamano hilo wanasema lengo lilikuwa kuanzisha njia mpya kati ya Sierra Leone na wawekezaji wa kimataifa, kwa kuzingatia uendelevu, miundombinu na ushirikiano wa muda mrefu.
Uzito wa historia
Njia ya Sierra Leone hadi kufika mkutano wa Istanbul imepitia njia ngumu. Vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoonekana kutoisha vilivyoikumba nchi hiyo kuanzia mwaka 1991 hadi 2002 vilisababisha vifo vya zaidi ya watu 50,000 na wengine milioni 2.5 kuyahama makazi yao, idadi ambayo ni ya kushangaza kwa taifa la watu milioni 4.5 wakati huo.
Kufikia 1991, Sierra Leone iliorodheshwa kati ya nchi masikini zaidi ulimwenguni, na Benki ya Dunia.
Mzozo huo, ambao kimsingi ulifadhiliwa na "almasi za damu" ambao ulichochea mateso ya wanadamu, uliharibu sio tu miundombinu bali hata muundo wake wa kijamii. Zahanati nyingi ambazo serikali ilikuwa imeanzisha zilibomolewa kabisa.
Kizazi kizima cha vijana, walinyimwa elimu pale mfumo wa shule ulipoporomoka, wakawa rahisi kujiunga na majeshi ya waasi.
Nchi ilipokuwa ikijaribu kuinuka tena, mzozo mwingine ulitokea. Mlipuko wa Ebola wa 2014-2016 uliharibu uchumi ambao tayari ulikuwa dhaifu. Kufikia 2016, Benki ya Dunia ilikuwa imepunguza makadirio ya ukuaji wa Sierra Leone hadi 0.3%, chini zaidi kutoka kwa makadirio ya kabla ya Ebola.
Kufufuka kwa Sierra Leone
Data iliyotolewa hivi majuzi inaashiria uwezekano wa kuimarika kwa uchumi wa Sierra Leone.
Sekta ya madini ina nafasi muhimu katika uchumi wa nchi, ikichangia takriban asilimia 7 ya Pato la Taifa ambayo ni takribani asilimia 80 ya mauzo ya nje, kulingana na ripoti ya 2024 ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).
Baomahun iliyoko katika eneo la Bo na Tonkolili ina rasilimali inayotii Kanuni za Kamati ya Akiba ya Pamoja ya Ore ya wakia milioni 5.8 na inatarajiwa kuanza kuzalishwa mwaka huu, ikilenga wakia 185,000 kila mwaka.
Kuimarika kwa sekta ya madini kumechangia kuimarika kwa uchumi zaidi. Ukuaji unatarajiwa kuimarika hadi asilimia 5.2 mwaka 2025, ukichochewa na sekta ya madini na kuimarika kwa kilimo, viwanda, ujenzi na utalii, kulingana na Benki ya Maendeleo ya Afrika.
"Jambo la kwanza tulilofanya ni kuanzisha na kutekeleza idadi kubwa ya mageuzi ambayo yanaathiri biashara na uwekezaji. Unahitaji kupata mfumo sahihi wa udhibiti ili kuweza kuvutia wawekezaji," Waziri wa Biashara na Viwanda wa Sierra Leone, Ibrahim Alpha Sesay, ameiambia TRT Afrika.
"Wiki chache zilizopita, mapitio yetu ya tatu ya sera ya biashara yaliwasilishwa katika Shirika la Biashara Duniani (WTO), na tulikuwa na mapitio mazuri sana. Tunatarajia idhini hiyo kuja wakati wowote kuanzia sasa, kwa hivyo hii inaonyesha nia yetu ya kuwa sehemu ya mfumo wa biashara duniani."
Hivi majuzi Sierra Leone ilirekebisha sheria yake ya uchimbaji madini ili kuifanya sekta hiyo kuwa ya kisasa na kuhakikisha faida kubwa kwa umma.
Msingi ni Sheria ya Maendeleo ya Migodi na Madini ya mwaka 2022, ambayo ilichukua nafasi ya sheria ya mwaka 2009 na kuanzisha sheria kali za uchunguzi, uendeshaji na biashara ya madini.
Marekebisho hayo yanaenea zaidi ya uchimbaji madini. Sierra Leone imejiunga na Mpango wa Uwazi wa Viwanda vya Uziduaji, kutekeleza Mchakato wa Kimberley wa uidhinishaji wa almasi, na kuanzisha Wakala wa Kitaifa wa Madini ili kuimarisha usimamizi na uwajibikaji ndani ya tasnia ya uziduaji.
Sekta ya utalii, ambayo imefunikwa kwa muda mrefu na tasnia ya uziduaji, inaibuka kama kichocheo kingine muhimu cha ukuaji.
Mapato ya sekta ya utalii yanatarajiwa kupanda hadi takriban $109 milioni ifikapo 2028, kutoka $91 milioni mwaka 2023.
Zaidi ya madini
Makampuni ya ujenzi na utengenezaji wa Uturuki yanazidi kufanya kazi nchini Sierra Leone, yakiungwa mkono na dhamira ya Rais Recep Tayyip Erdogan ya kudumisha ushirikiano uliopo na nchi za Afrika kupitia kile kinachoelezewa rasmi kama ushirikiano wa "ushindi kwa wote."
"Sierra Leone ni soko zuri sana kwa wawekezaji wa biashara wa Uturuki. Idadi ya watu ni vijana, ambayo inatafsiriwa kuwa wafanyakazi wenye tija zaidi ambao pia wanaweza kujifunza na kuendeleza. Tunafurahi kufanya biashara hapa," Faruk Deveci, mwakilishi wa Baraza la Biashara la Kituruki Duniani nchini Sierra Leone, ameiambia TRT Afrika.
Kulingana na Deveci, ujenzi ni kati ya sekta zenye nguvu zaidi za uchumi.
"Watu wa Sierra Leone wanawekeza katika nyumba, ikiwa ni pamoja na kupangisha. Wanajenga upya nchi yao, huku ujenzi ukishikilia ufunguo wa uchumi kukua," anaelezea.
Ufikiaji wa kidiplomasia unaongeza uhusiano wa kibiashara kati ya Uturuki na Sierra Leone. Ubalozi wa Uturuki mjini Freetown, mji mkuu wa Sierra Leone, ulianza kazi tarehe 1 Februari 2018. Miaka miwili baadaye, Sierra Leone ilifungua ubalozi jijini Ankara.
‘’Kiwango cha biashara baina ya nchi mbili mwaka 2017 kilipanda kutoka dola milioni 51.5 hadi dola milioni 55.3 za Marekani mwaka 2018. Kiwango cha biashara baina ya nchi mbili kilirekodiwa kuwa dola milioni 53,4 mwaka 2019. Bidhaa kuu zilizosafirishwa kutoka Uturuki ni unga, sukari, chuma, saruji, bidhaa mbalimbali za chakula, waya za kebo, na plastiki za kufinikia . Bidhaa zinazoagizwa kutoka Uturuki zinajumuisha zaidi titani na bidhaa za ngozi,’’ Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki ilisema kwenye tovuti yake.
‘’Shirika la Ndege la Turkish Airlines husafiri kutoka İstanbul hadi Freetown mara 3 kwa wiki. Kupitia Shirika la Ushirikiano na Uratibu la Uturuki (TİKA), Uturuki inatoa usaidizi wa maendeleo kwa Sierra Leone katika nyanja mbalimbali. Tangu 1992, serikali ya Uturuki imekua ikitoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi kutoka Sierra Leone.’’
Safari ya kuimarisha miundombinu
Wajumbe katika mkutano wa Istanbul walibainisha mapungufu katika miundombinu, upatikanaji wa nishati na utoaji wa huduma kama maeneo ambayo yanahitaji uangalizi wa haraka wa serikali ya Sierra Leone.
"Tunajua nishati ni changamoto kuu, tumepiga hatua katika suala la nishati, tumeongeza uzalishaji wetu wa nishati ya kijani. Pia tumeongeza idadi ya watu wanaopata umeme. Hata hivyo bado hatujafikia malengo yetu. Inaweza kuwa bora zaidi, lakini hiyo ni dhamira kubwa aliyoitoa Mheshimiwa (Rais Julius Maada Bio)," Sesay aliiambia TRT Afrika.
Serikali imeongeza karibu mara mbili uwezo wa kuzalisha umeme hadi megawati 253 katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, lakini mahitaji ni makubwa.
Kwa wawekezaji wa kimataifa, Sierra Leone inatoa fursa kubwa. Rasilimali hizo haziwezi kukanushwa - kutoka kwa kiwango cha juu cha ardhi hadi kilimo na fukwe safi zinazofaa kwa maendeleo ya utalii.
Ajenda ya mageuzi ya serikali inaonekana kuwa ya kweli, ikiungwa mkono na washirika wa kimataifa, ikiwa ni pamoja na Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afria (AfDB).