Tanzania yavisha mifugo hereni za kielektroniki, wafugaji kunufaika na soko la kimaitaifa
AFRIKA
3 dk kusoma
Tanzania yavisha mifugo hereni za kielektroniki, wafugaji kunufaika na soko la kimaitaifaHatua hiyo inalenga kujua takwimu za mifugo, kuboresha miundombinu ikiwemo malisho na kuondoa nadharia za mazoea kwa baadhi ya wafugaji.
Hatua hiyo inalenga kujua takwimu za mifugo, kuboresha miundombinu ikiwemo malisho. Picha/TRT Afrika / TRT Afrika Swahili
3 Julai 2025

Maelfu ya wafugaji nchini Tanzania wanatarajiwa kuanza kunufaika na masoko ya nyama kimataifa, baada ya Serikali ya nchi hiyo, kuanza rasmi kuchanja na kuvisha mifugo hereni za kielektroniki kama sehemu ya kuthaminisha mifugo kimataifa, na wafugaji kukopesheka katika taasisi mbalimbali za kifedha.

Miongoni mwa vikwazo vilivyokuwa vinakwamisha jitihada za wafugaji, ni kukosekana kwa ithibati kutoka Shirika la Afya ya Wanyama Duniani (WOAH).

Tanzania ambayo inatajwa kuwa ya pili kwa mifugo Afrika baada ya Ethiopia haikuwahi kunufaika na mifugo yake tangu uhuru wa nchi hiyo.

Hatua hiyo inalenga kujua takwimu za mifugo, kuboresha miundombinu ikiwemo malisho na kuondoa nadharia za mazoea kwa baadhi ya wafugaji kama Yohana Ole Murumba ambaye alitumia njia za kienyeji kutibia mifugo, kama kupiga chapa ya mto na kuharibu taswira ya ngozi na wakati mwingine kusababisha vifo kwa baadhi ya mifugo yake.

“Kwa sasa ninafuraha kwa sababu naamini tiba hii inayotolewa na Serikali itatibu mifugo yetu kabisa,” amesema Mrumba.

“Tabu tuliokuwa tunapata ni kwamba kuna wakati mifugo inaugua na kuharisha damu, na sisi tunaitibu kwa njia za kienyeji kiasi kwamba hatukuwa na uhakika wa mifugo kupona, lakini sasa tuna uhakika na utaratibu wa Serikali.”

TRT Afrika ilitembelea kijiji cha Engikaret Wilaya ya Longido Mkoani Arusha, miongoni mwa maeneo yalioanza utekelezaji wa zoezi hilo na kukutana na Sendi Mutara aliyepeleka mifugo yake kwa ajili ya chanjo na hereni.

Mutura aliiambia TRT Afrika kwamba mifugo kwa jamii ya Kimasai ni kama benki kwa kabila hilo.

“Tunafurahia sana. Unajua mtu anayependa mifugo ni kama benki kwetu sisi wamasai,” amesema.

Hata hivyo, Dkt. Benezeth Lutege Malinda anayewakilisha Shirika la Afya ya wanyama Duniani (WOAH) anasema hatua hii ni ya kulinda thamani ya afya ya binaadamu kutotumia mazao ya mifugo ya wanyama ambao hawajapata tiba sahihi.

“Unajua hereni hizi zina taarifa zote za nchi, na hereni hizi hulinda taarifa za mnyama tangu anapozaliwa na huduma zote alizozipata kwa kipindi cha maisha yake na kwa sababu hiyo inaiwezesha serikali kufanya ufuatiliaji wa kina,“ alisema.

Zoezi hilo ambalo lilizinduliwa na Rais wa nchi hiyo, Samia Suluhu Hassan katikati mwa mwezi Juni mwaka huu linasimamiwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Waziri anayesimamia Wizara hiyo Dkt. Ashatu Kijaji ameviambia vyombo vya habari vya ndani na nje kuwa masoko ya Ulaya, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) zipo tayari kununua mifugo hiyo ikiwa hai.

Anasema Wizara hiyo kupitia kitengo cha mashirikiano kati ya Sekta binafsi na Serikali imeanza hatua za ushiriakano na baadhi ya wale walioonesha utayari.

“Hatukuwa tumechanja mifugo yetu kitaifa na hatukuwa na takwimu za mifugo, lakini leo hii nimetoka kusema mwaka huu pekee tunatakiwa kupeleka tani elfu hamsini na nne kwa soko la China na nchi ya Misri tumeanza majadiliano nao,” amesema Dkt. Kijaji.

Ikiwa zoezi hili litakamilika ndani ya kipindi cha miaka mitano kama lilivyopangwa na Serikali, inamaanisha kwamba ng’ombe takriban Milioni 19, mbuzi na kondoo milioni 17 na kuku milioni arobaini watakuwa wamefikiwa.

Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us