Serikali ya Iran imetangaza kufungua anga lake, baada ya kuifunga kuanzia Juni 13, kufuatia mashambulizi kati yake na Israel.
"Viwanja vya ndege vya kimataifa vya Mehrabad na Imam Khomeini, pamoja na vile vilivyopo kaskazini, mashariki, magharibi na kusini mwa nchi vimefunguliwa, tayari kuhudumia ndege,” kilisema chombo cha habari cha nchi hiyo IRNA, siku ya Alhamisi.
Kulingana na IRNA, safari za ndani na nje ya Iran, isipokuwa zile zitakazohusisha miji ya Isfahan na Tabriz, zitaendelea kuanzia saa 11 asubuhi hadi saa 12 jioni.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa, safari za ndege katika miji hiyo miwili, zitarejea mara baada ya marekebisho ya miundombinu.
Iran ilifunga anga yake mwezi uliopita, baada ya Israel kufanya mashambulizi mfululizo, hatua iliyoilazimu nchi hiyo kujibu mashambulizi.
Hata hivyo, makubaliano ya kusitisha vita hivyo yalifikiwa Juni 24, mwaka huu.