Soka yarejea Somalia: Eto'o, Adebayor, Okocha waingia uwanjani
Soka yarejea Somalia: Eto'o, Adebayor, Okocha waingia uwanjani
Samuel Eto’o, Emmanuel Adebayor, na Jay-Jay Okocha waliongoza mechi hiyo huku soka la Somalia likiwa na ndoto ya kufufuka baada ya vita. Ni njia ya nchi kuuambia ulimwengu wa michezo: Tumerudi.
28 Mei 2025

Mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, ulikuwa mwenyeji wa mechi yake ya kwanza ya hadhi ya juu ya soka tangu kuzuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe zaidi ya miongo mitatu iliyopita, huku magwiji wa Kiafrika wa mchezo huo wakiingia uwanjani kwa mechi ya maonesho dhidi ya wenzao wa Somalia.

Mechi hiyo ilichezwa siku ya Jumanne katika uwanja wa Mogadishu na ilishirikisha wachezaji soka nyota wa zamani wa Afrika kama Samuel Eto’o wa Cameroon, Emmanuel Adebayor wa Togo na Jay-Jay Okocha wa Nigeria.

Ilipewa jina la Ziara ya Kihistoria ya Amani, ikisisitiza matumaini ya Somalia kurejea katika ulimwengu wa kimataifa wa soka. Wajumbe wa FIFA na shirikisho la soka barani Afrika CAF pia wanatarajiwa kuzuru nchi hiyo hivi karibuni.

Shirikisho la Soka la Somalia lilisema kuwa mechi hiyo ya maonesho pia ililenga kubadilisha mitazamo ya kimataifa ya utulivu na utayari wa nchi kujiunga tena na jumuiya ya kimataifa ya michezo.

Kuimarisha hadhi

"Somalia kuwa na uwezo wa kuandaa mechi katika uwanja wa Mogadishu ni msaada mkubwa wa kuimarisha hadi yetu ya soka," alisema Ali Abdi Mohamed, Rais wa Shirikisho la Soka la Somalia.

"Lengo ni kuonesha kwamba viwanja vyetu viko tayari kuandaa mechi za kiwango cha juu. Tunataka kutambua mapungufu yaliyosalia ili kufikia viwango vya kimataifa," aliongeza.

Wakati mmoja uwanja wa Mogadishu ulikuwa miongoni mwa uwanja mkuu wa soka wa Afrika Mashariki na uliandaa mashindano makubwa yaliyokuwa na mashabiki wengi kama vile Kombe la CECAFA la 1977.

Imegeuka kambi ya kijeshi

Lakini iligeuzwa kambi ya kijeshi wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe, na wakati fulani iliwakaribisha walinda amani wa Umoja wa Mataifa na wanajeshi wa vikosi vya Umoja wa Afrika nchini Somalia (Amisom) ambao walipelekwa huko kulinda serikali.

Ilifunguliwa tena mnamo 2020 kufuatia kufanyiwa ukarabati ili kuimarisha hali yake.

"Kwa kuwakaribisha wachezaji wa aina hii, lengo letu ni kuhimiza na kushawishi juu ya uwezo wa Somalia kuandaa mechi za kimataifa - zote za klabu na kitaifa," alisema Mohamed. "Imekuwa muda mrefu tangu tumeandaa mechi ya kiwango hiki."

Mashabiki waliruhusiwa kuingia kwenye mechi hiyo bila malipo huku maelfu ya mashabiki wakitarajiwa kuhudhuria. Usalama uliimarishwa maeneo ya karibu na ukumbi huo.

Mkutano na Rais

Magwiji hao wa soka wa Afrika walitarajiwa baadaye kutembelea ikulu ya rais kukutana na Rais Hassan Sheikh Mohamud.

"Tunatumai watu wa Somalia watasaidia kubadilisha taswira, kuhudhuria kwa wingi na kuonesha uungwaji mkono wao," alisema rais wa SFF. "Watu wetu wanastahili kupata burudani ya soka. Vijana wetu wanastahili kuwa tena na matumaini."

CHANZO:TRT Afrika
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us