Rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Joseph Kabila siku ya Alhamisi, Mei 29, alikutana na wawakilishi wa madhehebu ya kidini mashariki mwa DRC inayodhibitiwa na waasi.
Waasi wa M23, ambao wamekuwa wakipigana tangu mwishoni mwa 2021, walichukua udhibiti wa Goma Januari 2025. Na kufikia mwezi Februari walikuwa wanadhibiti mji wa Bukavu.
Ni takriban siku tatu baada ya Kabila kurejea Goma, mji mkuu wa Mkoa wa Kivu Kaskazini, na kufikisha kikomo cha miaka sita cha kuishi uhamishoni.

Katika ujumbe kupitia mtandao wa X, akitangaza mkutano huo, msemaji wa waasi wa Alliance Fleuve Congo (AFC/M23) Lawrence Kanyuka alimtaja Kabila kama "Rais wa Heshima."
Kurudi kwake Goma kunakuja siku mbili tu baada ya kuishutumu serikali ya Rais Felix Tshisekedi kwa uwongo, kiburi, kuweka taasisi za ukabila na upendeleo, na kutojali, miongoni mwa maovu mengine, ambayo alidai yaliharibu mshikamano wa kitaifa na kuifanya nchi kuwa dhaifu zaidi.
Kabila, 53, alitawala DR Congo kati ya 2001 hadi Januari 2019, na baadaye Rais Tshisekedi akachukua uongozi.
Baadaye wawili hao walitofautiana, huku Kabila akimshutumu Tshisekedi kwa kukiuka makubaliano yaliyomuingiza madarakani. Tshisekedi amemshutumu Kabila kwa kuwaunga mkono waasi wa AFC/M23.
Kabila alijiuzulu baada ya takriban miaka 20 madarakani mwaka 2018.
Amekuwa nje ya nchi tangu mwishoni mwa 2023, hasa Afrika Kusini.
Bunge la Seneti liliunga mkono kumuondolea kinga yake ya urais kwa kura 88 kwa 5 kupitia kura ya siri.
Rais huyo wa zamani, ambaye alimaliza ukimya wake juu ya mzozo nchini DRC mwezi Februari mwaka huu, hapo awali amemshutumu Tshisekedi kwa kusimamia vibaya mgogoro wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na akatupilia mbali majaribio ya rais huyo kuwalaumu wahusika wa nje kwa hilo.
Kurudi kwake katika mji wa Goma kunaweza kuashiria sura mpya katika mzozo kati ya rais Tshisekedi na waasi wa M23, ambao wamedhibiti maeneo mengi, ikiwa ni pamoja na Bukavu, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kusini, tangu mapema 2025.