Marufuku ya wamiliki wa usafiri wa umma inavyoathiri vipato vya wasafirishaji binafsi
AFRIKA
3 dk kusoma
Marufuku ya wamiliki wa usafiri wa umma inavyoathiri vipato vya wasafirishaji binafsiUganda imepitisha sera mpya ya serikali ya kupiga marufuku wawekezaji binafsi katika usafiri wa umma. Sera hiyo mpya inafuatia kuongezeka kwa ajali za barabarani ambazo zinahusishwa na magari yaliyo katika hali hatari ya kiufundi na utovu wa nidhamu
Uganda kupiga marufuku umiliki wa usafiri wa abiria na watu binafsi/ picha: TRT Afrika / TRT Afrika Swahili
28 Mei 2025

Na Eudes Ssekyondwa, Kampala, Uganda

Kwa zaidi ya miaka kumi na mitano, shughuli ya ubebaji abiria ndani ya jiji la Kampala, imekuwa chanzo kikubwa cha mapato kwa Ali Kabuye. 

Kabuye aliweza kununua gari lenye uwezo wa kubeba abiria 14, kwa njia ya mkopo. 

Hata hivyo, hofu kubwa imetawala akili yake kwa sasa, kufuatia agizo la serikali ya nchi hiyo la kuzuia umiliki binafsi wa magari hayo.

"Tuna mifumo yetu ya kuweka akiba na tayari tunao wadhamini wa mikopo katika biashara hii,” anaiambia TRT Afrika.

“ Pendekezo la kujiunga na miradi mipya na kununua magari mapya ni njama ya kutuondoa kwenye biashara, kwa sababu magari mapya yaliyonunuliwa kwa mkopo yatatufanya kuwa wafanyakazi wao, ukipata dharura huwezi kutumia fedha zao," anaeleza.

Serikali ina lengo la usalama

Mei 12, 2024, serikali ya Uganda ilitangaza kuwa biashara ya kusafirisha abiria jijini Kampala na maeneo mengine ya nchi hiyo, yahusishe wamiliki wa vikundi peke yake.

Mpango huo unahusisha magari ya abiria 14 pamoja na mabasi.

Kulingana na serikali ya nchi hii, uamuzi huo unalenga kuimarisha usalama barabarani. 

Takwimu za serikali zinaonesha kuwa, wastani wa watu 14 hupoteza maisha kila siku kutokana na ajali za barabarani.

"Walijaribu hapo awali na hata kuanzisha mabasi maalumu pamoja na magari mengine ya umeme kwa lengo la kutuondoa kwenye biashara,”, anaeleza huku akisimamisha gari lake ili ashushe abiria.

Katika kituo cha magari ya abiria cha Busega jijini Kampala, kelele zimetawala, huku magari yakielekea pande tofauti. Baadhi yanapakia abiria, mengine yakianza safari huku mengine yakiingia kituoni hapo.

Maelfu ya magari haya yanamilikiwa na watu binafsi.

Na kanuni za uendeshaji hapa zinaamuliwa na wamiliki wenyewe.

"Tatizo kubwa katika serikali yetu ni upendeleo,” anasema Badru Ssentamu, mmoja wa wamiliki wa magari ya abiria.

“ Unapata pale waziri au mtu yeyote anapoanzisha kampuni yake wanataka kulazimisha kila mtu ajiunge na hiyo kampuni. Hiyo inamgusa mmiliki binafsi, hizi zote ni changamoto za ushindani.”

Taratibu za magari yanayomilikiwa na vikundi

Takriban wamiliki wa magari 400,000 waliopo jijini Kampala wataathirika na mabadiliko ya sheria kuhusu umiliki wa magari ya abiria.

Hata hivyo, kwa wengine, tayari wamekuwa nao utaratibu huo kwa muda.

"Niliianza zamani sana ingawa imekuwa safari ngumu na washindani wangu lakini ninaipenda na abiria wanathamini,” Peter Kagwa mwenyekiti wa kampuni ya Fly Express Entebbe Kampala anasema.

Kagwa anaongoza kikundi kinachomiliki magari 250 chini ya kampuni ya Expressway Entebbe

"Wazo hili lilianzishwa na serikali ili kuboresha mfumo wetu wa usafiri na kupanga jinsi watu wanavyokaa. Walialika kila mtu na kuwafundisha waliokwenda lakini wengine hawakulichukulia kwa uzito. Ilinifanya nikabadilisha biashara yangu ya usafirishaji, " Kaggwa anaeleza.

Chama chao kina kanuni wazi za maadili ili kuendelea kuvutia wateja katika soko hili lenye ushindani mkubwa. 

Kwa mfano, mbali na kuwa na vitambulisho, madereva pia wanashurutishwa kupitia mafunzo maalumu, huku wasaidizi wao wakitakiwa kuvaa sare rasmi wanapokuwa kazini. 

Kwa magari haya ya chama lazima abiria kupitia taratibu za usalama kabla ya kupanda.

Na hii Hiki ni kivutio kwa baadhi ya abiria.

"Teksi hizi ni za kipekee kwa sababu abiria wanapokaa hazipakii kupita kiasi. Lakini katika usafiri mwingine ambao haujadhibitiwa vyema hupakia abiria kupita kiasi na hii inaweza kuwa chanzo cha ajali kukithiri, "Shamim Nalwadda ambaye anasema huku akichnguzwa ma afisa wa usalama mlangoni pa gari.

Serikali ya Uganda kwa sasa inaendelea na ukaguzi wa taratibu, nambari za kidijitali za magari na utekelezaji wa kanuni za maadili kwa madereva. 

Lakini kwa ambao wamezoea umiliki binafsi, pengine itawachukua muda mpaka kuzoea utaratibu huu mpya.

Huku wengine, wanasubiria kuona, iwapo mara hii, serikali itafanikiwa katika utekelezaji wake tofauti na ilivyokuwa awali?

CHANZO:TRT Afrika Swahili
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us