Mamdani ambaye alizaliwa Kampala, Uganda mwaka 1991 ni mwanasiasa kijana na ana asili ya kutoka India.
Alihamia Marekani akiwa na umri wa miaka 7 na akaishi katika eneo la Astoria, jijini New York.
Ni mtoto wa mtayarishaji wa filamu kutoka India, Mira Nair, na Profesa Mahmood Mamdani, msomi wa siasa na historia kutoka Uganda.
Mamdani alichaguliwa kuwa mjumbe wa Bunge la Jimbo la New York mwaka 2020 kupitia chama cha Democratic Socialists of America (DSA), na hivi karibuni ameshinda mchujo wa chama cha Democratic kwa nafasi ya Meya wa New York, akimshinda aliyekuwa gavana wa New York Andrew Cuomo.
Sasa akisubiri uchaguzi mkuu ambao utafanyika mwezi Novemba 2025.
Ana matumaini makubwa kutokana na kuungwa mkono pakubwa na vijana, wahamiaji, na wapiga kura wa mrengo wa kushoto, huku wapinzani wake Cuomo na Eric Adams wakigombea kama wagombea wa kujitegemea na huenda kura zao zikagawanyika.
Baadhi ya sera zake kuu ni kama usafiri wa umma wa bure na kodi nafuu za nyumba, sera ambazo zimepewa jina la “Zohranomics.”
Mamdani pia ameunga mkono hadharani harakati za Wapalestina, msimamo uliozua mjadala mkubwa na kumpatia pia ukosoaji kutoka kwa viongozi kama Donald Trump, ambaye amemtishia kumrudisha ''kwao'' ikiwa ataendelea kutetea haki za wahamiaji.
Anafananishwa na Barack Obama kwa sababu ya asili yake ya Afrika Mashariki, mvuto wake kwa kizazi kipya, uwezo mkubwa wa kuhamasisha, na kuonekana kama kiongozi mpya mwenye ajenda ya mabadiliko.
Iwapo atashinda, atakuwa Meya wa kwanza Muislamu katika historia ya jiji la New York.
