Balozi wa Israel nchini Senegal, Yuval Waks, alilazimika kuondoka katika chuo kikuu cha Dakar siku ya Jumanne baada ya wanafunzi kupinga uwepo wake na kuimba nyimbo za kuunga mkono Palestina, kulingana na picha zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii.
Waks alikuwa amealikwa kuhutubia katika mkutano kuhusu mazoea ya mahusiano ya kimataifa katika Chuo Kikuu cha Cheikh Anta Diop (UCAD), taasisi kubwa na maarufu zaidi ya elimu ya juu nchini.
Lakini alipofika, makumi ya wanafunzi walikusanyika nje ya ukumbi, wakiimba "Palestine Huru", "Gaza Huru" na "Israel ni mhalifu wa kivita".
Video zilizoshirikiwa mtandaoni zinaonyesha wanafunzi wakipeperusha bendera za Palestina na kumzomea mjumbe huyo mpya, na kumzuia kutoa hotuba yake.
Ndiye Balozi wa Israel katika nchi 6
Waks alisindikizwa na usalama na kuondoka chuoni bila kuhutubia hadhira. Waandamanaji waliendelea kumfuata huku wakipiga kelele na kupeperusha bendera alipokuwa akiondoka.
Waks, ambaye pia anahudumu kama balozi asiye mkaaji wa Israel nchini Gambia, Guinea, Guinea-Bissau, Cape Verde na Chad, aliwasilisha hati zake za utambulisho kwa Rais wa Senegal Bassirou Diomaye Faye mnamo Mei 8.