AFRIKA
2 dk kusoma
Marekani yajadili na DRC mikataba ya madini yenye thamani ya mabilioni
Haijafahamika ni jinsi gani Marekani itatekeleza mikataba hiyo Congo, lakini mshauri mwandamizi wa Rais Donald Trump kwa Afrika amesema kwamba kampuni za Marekani zitashirikishwa.
Marekani yajadili na DRC mikataba ya madini yenye thamani ya mabilioni
Muonekano wa migodi ya shaba na kobalti kaskazini magharibi mwa Lubumbashi nchini Congo. / Reuters
4 Aprili 2025

Marekani ipo katika mazungumzo ya kuwekeza mabilioni ya dola katika nchi ya DRC yenye utajiri wa madini na inataka kusaidia kumaliza mgogoro unaoendelea katika eneo la mashariki ya nchi, amesema mshauri mwandamizi wa Rais Donald Trump kwa Afrika katika ziara yake siku ya Alhamisi.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambayo ina akiba nyingi ya madini ikiwemo kobalti, lithiamu na Urania, imekuwa ikipambana na vikosi vya M23 vinavyodaiwa kuungwa mkono na Rwanda ambavyo vimechukua sehemu kubwa ya eneo lake mwaka huu.

Hata hivyo, Rwanda imekuwa kipinga tuhuma hizo.

Marekani ambayo Jumatano wiki hii imeishangaza dunia kwa kutangaza ongezeko la asilimia 10 ya ushuru kwa bidhaa zote zitakazoingizwa nchini mwake, ilisema mwezi uliopita kwamba iko tayari  kushirikiana na DRC katika uchimbaji madini muhimu hasa baada ya mbunge wa Congo kuwasiliana na maafisa wa serikali ya Marekani na kupendekeza makubaliano ya madini kwa ulinzi.

“Bila shaka umesikia kuhusu makubaliano ya madini. Tumepokea pendekezo la Congo, na Rais na mimi tumekubaliana kuhusu utaratibu wa kuendeleza,” mbunge wa Marekani na mshauri Massad Boulous amesema baada ya kukutana na Rais wa Congo Felix Tshisekedi jijini Kinshasa.

Ushawishi wa China

Taarifa zaidi za mkataba huo, au pendekezo la Congo, hazikuwekwa wazi siku ya Alhamisi. Hata hivyo, shughuli za uchimbaji wa madini ya Congo ambayo pia yanatumika kutengeneza simu za mikononi na magari ya umeme, kwa sasa zimetawaliwa na China na kampuni zake za madini.

Haijafahamika ni jinsi gani Marekani itafanya kazi nchini Congo, lakini Boulos ameashiria kwamba kampuni za Marekani zitashirikishwa.

“Bila shaka, kampuni za Marekani zinafanya kazi kwa uwazi na zitachangia ukuaji wa uchumi. Huu ni uwekezaji wenye thamani ya mabilioni ya dola,” amesema.

Mazingira ya biashara

Joseph Bangakya, mbunge nchini Congo na rais wa kundi la wabunge marafiki wa Congo na Marekani, ameliambia shirika la Reuters kwamba wabunge wanaandaa muswada wa kukuza mazingira ya biashara ya nchi.

“Ni lazima kwa nchi yetu kufanikisha mikataba ya biashara na Marekani,” amesema.

Ameongeza kusema kuwa, Marekani inataka kusaidia kuleta amani mashariki mwa nchi ambapo maelfu wameuliwa huku wengine wakilazimishwa na M23 kuhama makazi yao. M23 mwaka huu wamedhibiti miji miwili mikubwa ya mashariki mwa Congo.

“Tunataka amani ya kudumu ambayo itazingatia uhuru wetu wa mipaka ya DRC,” amesema.

“Hakuwezi kuwa na maendeleo ya uchumi bila ulinzi.”

Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us