Mnamo mwaka 2020, paka mdogo mwenye macho ya kijani aliamua kufanya onyesho kubwa wakati wa mkutano wa Biden huko Pennsylvania.
Aliruka jukwaani, na kushika hisia za Mke wa rais , Jill Biden. Paka huyo wa shambani hatimaye akawa na makazi katika Ikulu ya Marekani. Anaishi maisha ambayo paka wengi wangeona tu kwenye ndoto.
Willow sio paka pekee aliyekuwa na bahati kama hiyo. Ulimwenguni kote, paka wamejipendekeza kwa njia yao katika baadhi ya maeneo ya kuvutia sana.
Ndio, kuna paka mashuhuri nchini Uingereza, haswa jijini London, ambaye anaitwa Larry.
Larry mwindaji wa Panya
Larry ni paka anayefanya kazi katika 10 Downing Street, ofisi rasmi ya Waziri Mkuu wa Uingereza.
Anajulikana kama "Chief Mouser" (Mwindaji Mkuu wa Panya), na alichukuliwa mwaka 2011 wakati wa uongozi wa Waziri Mkuu David Cameron ili kudhibiti tatizo la panya ofisini hapo.
Larry amekuwa maarufu sana, na watu wanamtembelea na kupiga picha kila wanapofika kwenye eneo hilo la kihistoria.
Larry pia amejizolea mashabiki duniani kote kwa tabia zake na picha zake zinazopigwa akiwa karibu na viongozi wa kisiasa wanaotembelea ofisi ya waziri mkuu.
Lilibet
Huko London, paka sio tu wanyama vipenzi - wao ni wafalme. Mfahamu Lilibet, paka mzuri wa misitu ya Siberia, na hata kupewa jina la Malkia Elizabeth II.
Lilibet amefanya makao yake katika hoteli ya nyota tano ya The Lanesborough.
Anapumzika kando ya moto, akinyosha miguu yake wakati wageni kutoka duniani kote wanakuja kumtazama.
Wengine hata hukodi vyumba katika hoteli hiyo ili tu kukutana naye. Kwa kweli yeye anavutia, anakufanya uhisi kama uko nyumbani katika mazingira hayo ya kifahari.
Na yeye sio paka pekee anayeishi maisha mazuri katika jengo la kihistoria la London.
Katika Kanisa Kuu la Southwark, paka anayeitwa Hodge amefanya chumba cha kanisa kuwa nyumbani kwake.
Amekuwa maarufu sana miongoni mwa wageni. Hata wanauza sanamu zake katika duka la zawadi!
Paka wa Venezuela
Na huko Venezuela, kuna paka anayejulikana kwa kuzunguka Baraza la Kitaifa la Uchaguzi huko Caracas.
Hata hivyo, hajishughulishi na siasa. Anapenda zaidi kucheza na waya za vipaza sauti na kuandamana na waandishi wa habari wanapongoja habari mpya.
Kisha kuna Lule, paka mpendwa huko Pristina, Kosovo. Lule anaishi katika Café Dit' e Nat, ambapo amekuwa maarufu sana hata kuchorwa uso wake kwenye vifuko vya sukari vya mgahawa.
Yeye ni zaidi ya mnyama kipenzi - yeye ni roho ya mahali hapo, anasema mmiliki wa mgahawa.
Paka wa Istanbul
Hata hivyo, sio kila paka maarufu ana ukoo mrefu au nyumba ya kifahari. Wengine tu hujitokeza, wanapata nafasi yao, na hawahami kamwe.
Paka mmoja mnene wa rangi ya kijivu na nyeupe wa mitaani kutoka Istanbul aliteka moyo wa mji - na umaarufu katika mitandao - kwa mtindo wake wa kusimama unao pendeza akiwa mitaa ya Kadikoy aliyepewa jina la Tombili.
Baada ya kifo cha Tombili, manispaa ya Kadikoy iliagiza sanamu kwa heshima yake.
Sanamu hiyo iliwekwa kwenye ngazi ambapo picha yake maarufu ilipigwa.
Kuanzia makao ya kifalme hadi mikahawa ya kupendeza na mitaa yenye shughuli nyingi, paka wamepata sehemu yao katika kila kona ya dunia, wakiacha athari mahali popote wanapokwenda.