Huku mioto nyika ikiendelea kuleta madhara makubwa sehemu tofauti duniani, mke wa Rais wa Uturuki Emine Erdogan amezitaka nchi tajiri ulimwenguni kugawana mzigo wa madhara ya mabadiliko ya tabia nchi.
Akigusia madhara hayo kwa nchi zinazoendelea, mke huyo wa rais amesema licha ya kwamba baadhi ya mataifa kuchangia chini ya asilimia moja ya hewa ukaa duniani, bado zinaendelea kupoteza rasilimali muhimu za chakula.
“Nchi haziwezi kuteseka peke yao,” alisema, akiitaka jumuiya ya kimataifa kutafuta suluhu ya utofauti huo, wakati akizungumza katika jukwaa maalumu la Sayansi ya Jamii huko Vatican.
Aligusia haja ya kuwa na mkakati madhubuti wa mabadiliko ya tabia nchi na kutokuwepo na taka, akizielezea kama hatua muhimu kuelekea kupata haki na uendelevu wa ubinadamu.
Alikosoa namna mifumo ya kiulimwengu ilivyoshindwa kugawana mizigo hiyo, akitoa wito kwa mashirika na taasisi mbalimbali duniani kulipa kipaumbele, mapambano ya mabadiliko ya tabia nchi.
Katika risala yake, mke huyo wa rais aligusia vuguvugu la ‘Kutokuwepo na Taka’, lililozinduliwa mwaka 2017, hadi kuwa mkakati wa kiulimwengu kupitia azimio la Umoja wa Mataifa.
Aliuelezea mkakati huo kama “heshima kwa utu”. “Hili si jukumu tu la kimazingira tu, bali kipimo cha kuhakikisha uwepo wa haki haki ya jamii na vizazi,” alisema.
Vuguvugu hilo linaashiria imani ya Uturuki ya kuilinda asili kama zawadi itokayo kwa Mungu.
Erdogan alisisitiza haja ya kuchanganya teknolojia na tunu za kimaadili ili kupata suluhu zenye kuleta mabadiliko.
Pia, alionya juu ya madhara ya kutoheshimu asili.
“Vuguvugu hili linaakisi jukumu la kimazingira linavyoendana haki ya jamii.
Erdogan alitoa wito wa mabadiliko ya kifikra yenye kuheshimu maendeleo ya mazingira.
Alihusisha janga la mazingira na masuala mengine kama vile umasikini, watu kukosa makazi na kukosekana kwa usawa ulimwenguni.
Kulingana na Erdogan, watu bilioni 3 wanaishi chini ya dola 5,50 kwa siku huku watu milioni 70 wakiishi kama wakimbizi, hali inayoashiria kushindwa kwa mifumo.
Alisisitiza kuwa changamoto hizo zinahitaji jitihada za pamoja zenye mshikamano ili kujenga dunia ya haki.
Erdogan aliangazia uongozi wa Uturuki katika masuala ya kibinadamu na kimazingira, akisema kuwa nchi hiyo imetoa hifadhi kwa wakimbizi wapatao milioni 4 kama sehemu ya mkakati wake wa kusaidia watu.