Baada ya kutokuwepo kwa siku 10 hali iliyozua wasiwasi kuhusu afya yake, Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir Mayardit amerejea nchini humo.
Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 73 aliwasili kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu akiwa na maafisa kadhaa wa serikali lakini hakuzungumza na umma.
Alipokelewa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Juba na viongozi wakuu wa serikali, akiwemo Makamu wa Rais Dk. Benjamin Bol Mel.
Safari ya Kiir katika taifa hilo la Ghuba, ambako alikaa siku 10, ilikuwa imezua uvumi mkubwa kwamba alikuwa mgonjwa.
Hata hivyo, mamlaka ya serikali yake imesisitiza kuwa yuko katika afya njema, na kuzima uvumi kuhusu afya yake ambayo ilikuwa imeenea wakati wa kutokuwepo kwake.
Katibu wa Habari wa Rais, balozi David Amuor Majur ameviambia vyombo vya habari kwamba Rais alikuwa amewasili tu katika mji mkuu wa Juba kufuatia safari rasmi ya Umoja wa Falme za Kiarabu.
"Tumewasili Juba sasa hivi kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu na rais. Sasa yuko Juba," alisema.
Rais Kiir aliondoka aliondoka 22 Juni 2025 kuelekea Umoja wa Falme za Kiarabu kwa ziara rasmi ya kidiplomasia kulingana na ofisi yake.
Ofisi hiyo wakati huo haikusema ziara hiyo ingechukua muda gani.