Ethiopia inasema kuwa imetia saini makubaliano ya fedha ya dola bilioni 1 na Benki ya Dunia siku ya Ijumaa.
Wizara ya fedha imesema kupitia mtandao wa Facebook kuwa mpango huo utakuwa kwa njia ya mkopo na misaada.
Fedha hizo zitasaidia juhudi za serikali katika kuhakikisha uthabiti kwenye sekta ya fedha, kuimarisha ushindani wa kibiashara na utumiaji mzuri wa raslimali, taarifa iliongeza.
Wiki hii Shirika la Fedha la Kimataifa la IMF liliidhinisha tathmini mpya ya nchi hiyo ya Afrika Mashariki ya mradi wa mkopo wa dola bilioni 3.4.
Mabadiliko nchini Ethiopia
Haya yanajiri huku kukiongezeka wasiwasi kuhusu matatizo ya sera hizo ambazo zinaungwa mkono na taasisi za kimataifa za fedha kwa uchumi wa Afrika, huku wanauchumi wakisema kuwa mfumo wa fedha wa dunia haupendelei bara la Afrika.
Shirika la IMF linasema kuwa ni muhimu kwa Ethiopia kuimarisha soko la uhawilishaji wa fedha za kigeni, kuongeza mapato ya ndani, na kudhibiti deni la nje.