Watu 5 wanahofiwa kufa, na wengine watatu kujeruhiwa vibaya baada ya helikopta ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda(UPDF) kuanguka na kulipuka jijini Mogadishu nchini Somalia.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Ulinzi ya Uganda, helikopta hiyo ilikuwa ni sehemu ya jeshi la Umoja wa Afrika la kulinda amani na kudumisha utulivu nchini Somalia (AUSSOM), ikiwa na usajili AUO-015.
Ajali hiyo, ambayo ilitoka majira ya asubuhi ya Julai 2, 2025 kwa saa za Afrika Mashariki, ilisababisha mlipuko mkubwa, na kuwaunguza vibaya marubani wa helikopta hiyo.
Helikopta hiyo ilikuwa katika operesheni zake za kawaida wakati tukio hilo lilipotokea, kwa mujibu wa taarifa ya UPDF.
Kikosi cha AUSSOM kilithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, na kusema kuwa helikopta hiyo, inayoendeshwa na kikosi cha UPDF, ilianguka umbali wa mita 200 kutoka kwenye njia ya kurukia ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Aden Adde, saa moja na nusu kwa saa za Afrika Mashariki.
Helikopta hiyo ilikuwa imetoka kuruka kutoka uwanja wa ndege wa Baledogle, takriban kilomita 90 kaskazini magharibi mwa mji mkuu wa Somalia.
Kishindo cha kuanguka kwa helikopta hiyo, kilisababisha mlipuko uliosababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu ya karibu na kuwajeruhi raia watatu, UPDF imesema.
Jeshi la Uganda limefutilia mbali uwezekano wa shambulio la nje, huku msemaji wa Jeshi Felix Kulayigye, akizungumza na shirika la habari la Xinhua, akisema kuwa kundi la wanamgambo wa al-Shabab wameondolewa kwa kiasi kikubwa kutoka jiji la Mogadishu.