Sauti za ngoma zinasikika.
Wakiwa wanatamba na jukwaa, wacheza ngoma hawa wanayarudi miondoko kwa hisia, huku wakishangiliwa na watu.
Hawa si wacheza ngoma wa kikundi fulani kilicholetwa hapa kwa ajili ya kutoa burudani, bali ni wakimbizi wa Burundi, waliotafuta hifadhi katika kambi za Nyarugusu katika wilaya ya Kasulu na kambi ya Nduta iliyopo Kibondo, ndani ya mkoa wa Kigoma nchini Tanzania.
Masahibu ya Warundi
Vijana hawa walikimbia machafuko ya kisiasa yaliyotokea nchini Burundi, mwezi Aprili mwaka 2015 baada ya aliyekuwa Rais wa Burundi kwa wakati huo, Pierre Nkurunziza kutaka kuwania kwa mara ya tatu uongozi wa nchi hiyo.
Ghasia zilizofuatia jaribio la mapinduzi ya kijeshi Mei 2015, zilisababisha mamia ya watu kuuawa, maelfu kupoteza makazi yao, na baadhi ya watu 420,000 kukimbilia nchi jirani, ikiwemo Tanzania.
Wakimbizi kurudi kwao
Ndani ya kambi hizo, kwa kutumia sanaa za majukwaani, taasisi iitwayo Babawatoto inashiriki kampeni ya kuwajengea wakimbizi hao uelewa wa kuona umuhimu wa kurejea makwao.
Ikiongozwa na Mgunga Mwa Mnyenyelwa, toka mwaka 2015, taasisi hiyo imekuwa ikikita kambi katika kambi hizo, ikijaribu kutumia sanaa za uraghibishaji kuwasaidia wakimbizi hao kurudi kwao.
“Lengo kuu la taasisi ya Babawatoto ni kukuza na kuendeleza vipaji vya sanaa kwa watoto, tukiamini kuwa sanaa ni chombo cha kubadilisha tabia, chombo cha ulinzi wa mtoto na pia njia mojawapo ya uponyaji, hasa kwa wale wanaopitia changamoto za kimaisha,” anasema Mwa Mnyenyelwa,” katika mahojiano yake na TRT Afrika.
Gwiji huyo wa sanaa za majukwaani, ambaye aliwahi kutamba kung’ara na kikundi cha Parapanda Arts Theatre cha nchini Tanzania, anasisitiza umuhimu wa sanaa kama pia chombo cha kumrejeshea mtu utimamu wa akili, hususani vijana wadogo wa Kirundi ambao wanaishi katika kambi hizo.
“Kumbuka hawa ni watu ambao wameona mengi, mengine ya kutisha na kuogopesha, na kwa namna moja ama nyingine, wameathirika kisaikolojia,” anaeleza.
Afua bora
Hali hii ilimlazimu Mwa Mnyenyelwa na taasisi yake kuwekeza nguvu kwenye kambi hizo kwa nia ya kuwasaidia vijana wadogo, kukata shauri na kurejea nchini Burundi.
“Tuna vituo maalumu ambapo wakimbizi huwa wanavitembelea, nasi tunawafundisha mbinu za uraghibishaji kupitia sanaa za maigizo, vikaragosi na ngoma,”anabainisha.
Kulingana na Mkurugenzi Mtendaji huyo wa taasisi ya Babawatoto, mbinu inayotumika kwenye vipindi hivyo sanaa shirikishi ambapo waraghibishi wenyewe hufanya utafiti wa jamii wanazotokea.
Mara baada ya tafiti zao, wakisaidiwa na wataalamu wa sanaa za majukwaani, waraghibishaji wao huandaa maonesho, yawe ya ngoma, mashairi au hata maigizo yenye kulenga kufikisha ujumbe wa umuhimu wa wakimbizi hao kurudi makwao.
“Lugha za Kirundi na Kiswahili hutumika sana wakati wa uraghibishaji na kwa kiasi kikubwa zimesaidia sana kufikisha ujumbe tarajiwa,” anaweka wazi.
Mafanikio
Kama anavyosema mwenyewe, kampeni hiyo imesaidia kwa kiasi kikubwa kuwashawishi baadhi ya wakimbizi wa Burundi, hasa vijana wadogo kurejea makwao.
Mbali na watoto, maonesho hayo pia yamewavutia watu wazima, na kuongeza ari na kasi ya kampeni hiyo.
“Kwa wastani, watoto wapatao 150 hutembelea vituo vyetu kwa siku, na hii inadhihirisha wazi umuhimu wa uwepo wetu kwenye kambi hizo za wakimbizi,” anasema.
Kwa mujibu wa Mwa Mnyenyelwa, tayari kampeni hiyo imewafikia zaidi ya watoto 200,000 kwa mafanikio makubwa.
Utayari
Mwa Mnyenyelwa anasema kuwa inatia moyo kuona mwamko wa wakimbizi hao, na utayari wao wa kutaka kurudi nchini mwao.
“Mara nyingine, hata viongozi wa juu kutoka Burundi wanafika kwenye vituo vyetu, wakisisitizia ujumbe wa kurejea makwao,” anaongeza.
Serikali ya Tanzania imekuwa ikitoa hifadhi kwa zaidi ya wakimbizi zaidi ya 110,000 kutoka Burundi, ambao wanaishi kati kambi za Nyarugusu na Nduta.
Mwaka jana, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani na Maendeleo ya Jamii na Usalama wa raia wa Burundi, Theofile Ndarufatiye alisema kuwa, tangu mwaka 2017 hadi kufikia 2024, jumla ya wakimbizi 1,070,607 walirejea nchini humo.
Kulingana na Ndarufatiye, katika kipindi cha Januari hadi Mei 2024 pekee, jumla ya wakimbizi 5,709 walirejea Burundi, huku zaidi ya wakimbizi 100,000 wakiwa bado wapo katika kambi ya Nduta na Nyarugusu.