Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan aliendesha kwa majaribio gari jipya lililozinduliwa la T10F sedan na watengenezaji wa taifa wa magari yanayotumia umeme ya Togg siku ya Jumamosi, kuashiria umuhimu wa Uturuki unaoimarika duniani katika kutengeneza magari yanayotumia umeme.
Rais Erdogan alikuwa ameongozana na Rais wa masuala ya Biashara na Viwanda wa Uturuki (TOBB) Rifat Hisarciklioglu, Mwenyekiti wa shirika la Anadolu Tuncay Ozilhan, Mwenyekiti wa shirika la Zorlu Ahmet Nazif Zorlu, Mwenyeiti wa kampuni ya Turkcell Senol Kazanci, na Mwenyekiti Shirika la Tosyali Fuat Tosyali.
Haya yanajiri wakati ambao Uturuki inapanda chati katika soko la utengenezaji magari ya umeme duniani.
‘Mafanikio makubwa’
Hivi karibuni, Uturuki imekuwa soko la nane duniani kwa mauzo ya magari ya umeme 2024, hasa kutokana na uzalishaji wa ndani ya nchi, kuwa na maeneo mengi ya ‘kuchaji’ umeme, na serikali kusaidia, kulingana na shirika la kufanya utafiti wa magari lenye makao yake Uingereza la New AutoMotive.
Mwaka uliopita, Uturuki ilifanya mauzo ya magari hayo ya EV 123,982. Mwezi Aprili 2025 pekee, nchi hiyo ilikuwa nafasi ya saba duniani, huku wakiuza magari 11,173 — zaidi ya Norway na Italia na kuwa soko linaloongoza la EV katika mataifa ya Mediterania. Disemba 2024 Uturuki ilikuwa na mauzo makubwa zaidi ya EV, ikiuza magari 17,894, na kuwa katika nafasi ya sita duniani mwezi huo.
Shirika la New AutoMotive limeeleza ukuaji wa Uturuki kama ‘‘mafanikio makubwa,” likibaini kuwa soko la magari yanayotumia betri za umeme limeimarika kwa zaidi ya asilimia 10 katika kipindi cha miezi minane mfululizo.
Kuimarika kwa soko la magari yanayotumia umeme Uturuki kunaonekana kama nguzo muhimu ya agenda yake ya kuhifadhi mazingira, huku gari aina ya Togg ikiwa na nafasi muhimu ya kubadilisha mtazamo wa mustakabali wa sekta ya utengenezaji magari.