Ibada ya Hajj kwa Waislamu inakaribia kuanza, huku mahujaji kutoka maeneo mbalimbali wakijiandaa kwa safari ya Saudi Arabia, kitu kimoja ambacho kipo akilini mwa wengi: je hali ya hewa itakuaje mwaka huu, na nini kifanyike ili kukabiliana na hali ya joto kali?
Takriban vifo 1,300 viliripotiwa Hajj ya mwaka jana, kwa mujibu wa takwimu rasmi za Saudia.
Hajj ni moja ya nguzo tano za dini ya Kiislamu, na Waislamu wote ambao wana uwezo wanashurutishwa kukamilisha ibada hiyo, mara moja katika maisha yao.
Muda wake, unategemea muandamo wa mwezi wa Kiislamu, ikisogea mbele kila mwaka na kalenda ya kawaida.
Kwa zaidi ya siku nne, mamilioni ya mahujaji watatekeleza msururu wa taratibu za ibada, kuelekea Siku ya Arafat, ambayo ndio kilele cha Hajj, ambapo mahujaji hukusanyika katika Mlima wa Arafat, eneo ambalo Mtume Mohammad (S.A.W) alitoa hotuba yake ya mwisho.
Mwaka huu, mamlaka ya Saudi Arabia imetangaza kwamba siku ya Arafat itakuwa Juni 5, ikifuatiwa na Eidu al-Adha Juni 6.
Kwa miaka sasa, ibada ya Hajj imesadifiana na msimu wa joto kali Saudia.
Mahujaji wa mwaka jana, wameshuhudia joto kali la nyuzi joto 51.8, lililosababisha vifo vya maelfu ya watu.
Wakala wa Habari wa Saudia, imenukuu Kituo cha Taifa cha Utabiri wa Hali ya Hewa, kikitabiri kuwepo kwa joto kali katika eneo tukufu mwaka huu, huku nyuzi joto ikipanda kati ya 40 na 47, kiwango cha chini kikiwa kati ya nyuzijoto 27 hadi 32, na vuguto kati ya asilimia 15 mpaka 60.
Utafiti wa mwaka 2019 uliochapishwa na jarida la sayansi la Geophysical Research Letter, umetahadharisha kwamba, kutokana na mabadiliko ya tabia nchi, na kubadilika kwa majira ya Hajj, mahujaji wanaweza kukabiliwa na hali ya joto kali ambayo itakuwa na athari kwa afya zao.
Kwa nini mshtuko wa moyo unaua
Vifo vitokanavyo na mshtuko wa moyo wakati wa hajj zinasababishwa na mambo kadhaa, Dkt. Imran Afzal, Daktari kutoka Pakistan mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 35 ameiambia TRT World.
“Ni mchanganyiko hatari-joto kali, hali kama vile ya kisukari na presha, na kuchelewa kutambua dalili na kupata msaada.”
Joto la mwili linapopanda ghafla na kwa haraka, uwezo wa mwili wa kupoza unapungua, ikisababisha kushindwa kwa baadhi ya viungo kufanya kazi.
Katika mazingira ya Hajj, uchovu unaweza kusababisha mshtuko wa moyo.
“Mahujaji wengi hulazimika kuwa katika mazingira magumu kwa sababu ya kutaka kukamilisha ibada. Lakini hiyo inaweza kusababisha madhara,” amesema.
Jinsi mahujaji wanavyoweza kujikinga
Wakati Saudi Arabia ikijaribu kuweka vituo vya maji, njia zilizozibwa juu, na mfumo wa kutoa ukungu, jukumu la kujikinga bado liko kwa mahujaji, hasa watu wazima na watoto, ambao wapo hatarini zaidi.
Dkt. Afzal anashauri kunywa maji kwa wingi, kutumia mianvuli au kofia pana, kupaka mafuta ya jua, kupumzika katika ya ibada katika maeneo yaliyozibwa, kuepuka kufunga wakati wa joto kali, kusafiri katika kundi, na kupanga matibabu na watoa huduma wa afya.
“Mahujaji wenye magonjwa sugu wanahitaji kuwa na mkakati mzuri kabla ya tatizo,” anasema Dkt. Afza.