AFRIKA
2 dk kusoma
Kenya yatoa kipaumbele kwa elimu katika bajeti yake 2025/2026
Bajeti ya 2025/26 nchini Kenya imependekeza elimu ipewe zaidi ya dola bilioni 5.4 kutumika katika ngazi zote za sekta ya elimu.
Kenya yatoa kipaumbele kwa elimu katika bajeti yake 2025/2026
Kenya ina mpango wa thamani ya dola bilioni 33.2 kwa mwaka 2025/26/ Picha: Reuters
13 Juni 2025

Waziri wa Fedha nchini Kenya John Mbadi mnamo Alhamisi, 12 Juni, 2025, aliwasilisha bajeti ya zaidi ya dola bilioni 33.2 (shilingi trilioni 4.29) katika Bunge.

Bajeti inaonyesha uwekezaji mkubwa katika elimu, afya, ulinzi, miundombinu, na ustawi wa jamii.

Elimu ilipata mgao mkubwa

Elimu ilipewa kipaumbele zaidi katika makadirio ya serikali kwa mwaka ujao wa fedha.

Bajeti ya 2025/26 nchini Kenya imependekeza elimu ipewe zaidi ya dola bilioni 5.4 (shilingi bilioni 702.7).

Tume ya Kuwaajiri Walimu Kenya itapata mgao mkubwa ikiwa zaidi ya dola bilioni 2.9 (shilingi bilioni 387.2), ikifuatiwa na elimu ya bila malipo ya Sekondari iliyowekewa zaidi ya dola milioni 400 (shlingi bilioni 51.9).

Elimu ya Sekondari ilipewa zaidi ya dola milioni 223 (shilingi bilioni 28.9), na mfumo wa mikopo kwa elimu ya juu (HELB) kupewa zaidi ya dola milioni 320 (shilingi bilioni 41.5).

Ufadhili wa masomo ya chuo kikuu na vyuo vya ufundi TVET, elimu ya msingi, na usimamizi wa mitihani pia umejumuishwa.

Sekta ya usalama

Sekta ya usalama ilipangiwa zaidi ya dola bilioni 3.5 (shilingi bilioni 464.8) katika bajeti ya 2025/26.

Jeshi la taifa (KDF), lilitengewa sehemu kubwa zaidi zaidi ya dola bilioni 1.5 (shilingi bilioni 202.3), likifuatwa na Idara ya Polisi zaidi ya dola milioni 970 (shilingi bilioni 125.7).

Idara ya Ujasusi imekadiriwa zaidi ya dola milioni 395 (shilingi bilioni 51.4), ikiwa ni pamoja na kuzingatia uimarishaji wa kwenda na wakati, uimarishaji wa uchunguzi, na ununuzi wa magari mapya.

Sekta ya usafiri

Usafiri ulitengewa zaidi ya dola bilioni 1.6 kutumika kwa ajili ya ujenzi wa barabara mpya na ukarabati wa zingine.

Sekta ya nishati itapata zaidi ya dola milioni 480 (shilingi bilioni 62.8), huku msisitizo ukiwa katika upanuzi wa gridi ya umeme na nishati ya jotoardhi.

Kilimo kilipata zaidi ya dola milioni 360 (shilingi bilioni 47.6), hasa kwa ruzuku ya mbolea na kukuza thamani ya mazao.

Sekta ya mawasiliano na teknolojia, ICT, ilitengewa dola milioni 98 (shilingi bilioni 12.7) kwa miundombinu ya kidijitali na mipango mahiri ya jiji kama vile Konza Techno City.

CHANZO:TRT Afrika and agencies
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us