AFRIKA
3 dk kusoma
Magaidi waua zaidi ya wanajeshi 30 Mali
Taarifa zinasema baada ya mauaji ya wanajeshi kadhaa katika eneo la Boulkessi katikati mwa Mali siku ya Jumapili, magaidi walifanya mashambulizi mengine Timbuktu Jumatatu.
Magaidi waua zaidi ya wanajeshi 30 Mali
Jeshi la Mali linasema limelazimika kurejesha vikosi vyake nyuma. / AP
2 Juni 2025

Kambi ya jeshi la Mali iliyoko katika mji wa Timbuktu ilishambuliwa siku ya Jumatatu na "magaidi" na milio ya risasi ilisikika, wanajeshi na maafisa wa eneo hilo waliliambia shirika la habari la AFP.

"Tunakabiliana na magaidi wanaoshambulia Timbuktu. Tunapambana nao," chanzo kimoja cha jeshi kilisema. "Kambi hiyo iliyoko katikati mwa mji ilishambuliwa," chanzo hicho kiliongeza.

Afisa mmoja wa eneo hilo alisema: "Magaidi waliwasili leo Timbuktu wakiwa na gari lililojaa vilipuzi. Gari lililipuka karibu na kambi (ya kijeshi). Bado kuna kufyatuliana risasi kunaendelea."

Maafisa wa Umoja wa Mataifa wameagizwa kupitia ujumbe "wajikinge" na "kuwa mbali na madirisha" kutokana na "ufyatulianaji risasi katika mji wa Timbuktu".

Mkazi mmoja alieleza kusikia "ufyatulianaji wa risasi mjini" ambao "unasemekana kutokea upande wa kambi (ya jeshi).‘‘

Mwandishi wa habari kutoka eneo hilo amesema kwa njia ya simu kuwa "mji unashambuliwa". "Asubuhi hii mji wetu ulishambuliwa na makundi ya magaidi. Ufyatulianaji wa risasi ulisikika karibu na kambi ya kijeshi na uwanja wa ndege. Sote tukarudi nyumbani," alisema.

Mji wa kale wa Timbuktu, ambao wakati mmoja ulifahamika kama "mji wa watakatifu 333" kwa Waislamu muhimu waliozikwa huko, ulikumbwa na uharibifu mkubwa ukiwa chini ya udhibiti wa makundi ya kigaidi kati ya 2012 and 2013.

Wanajeshi kadhaa wameuawa

Mashambulizi ya Jumatatu yanakuja huku kundi hilo lenye uhusiano na Al Qaeda ambalo linaendeleza shughuli zake katika eneo la Afrika Magharibi la Sahel likidai kuhusika na mashambulizi ya siku ya Jumapili katika kambi ya jeshi ambapo vyanzo viwili vinasema yalisababisha mauaji ya wanajeshi zaidi ya 30.

Inasemekana kuwa wanajeshi zaidi ya 400 wameuawa na magaidi tangu kuanza kwa mwezi Mei katika kambi na miji nchini Mali, Niger na Burkina Faso.

Kundi la JNIM limesema katika taarifa siku ya Jumapili kuwa limechukua udhibiti wa kambi ya Boulkessi katikati mwa Mali, karibu na mpaka wa Burkina Faso.

Jeshi la Mali linasema limelazimika kurejesha vikosi vyake nyuma.

"Wanajeshi wetu wengi wanapigana wengine mpaka mwisho, kutetea taifa la Mali," taarifa yake ilisema, bila kueleza idadi ya waliouawa.

Msemaji hakujibu kuhusu suala la idadi ya waliouawa, lakini vyanzo viwili vya usalama vinasema zaidi ya wanajeshi 30 wameuawa.

Chanzo cha baraza la manispaa huko Mondoro, karibu na kambi hiyo, kilisema kuwa wapiganaji "walivamia kambi nzima" na watu wengi wameuawa, shirika la habari la Reuters liliripoti.

Mashambulizi ya hivi karibuni

Video zilosambazwa mtandaoni zinaonesha wapiganaji kadhaa wakishambulia kambi yote.

Kundi la JNIM limedai kuhusika na mashambulio kadhaa katika kanda hiyo.

Tarehe 24 Mei, linasema lilishambulia kambi moja huko Dioura, katikati mwa Mali, na kuwaua wanajeshi 40.

Siku ya Ijumaa, linasema lilidhibiti kambi ya Sirakorola kusini magharibi mwa Mali, ingawa jeshi linasema lilifanikiwa kukabiliana na shambulizi hilo. Halikueleza idadi kamili ya waliouawa katika tukio hilo.

Katika nchi jirani ya Burkina Faso, kundi la JNIM lilidai kuwa mashambulizi katika maeneo ya wanajeshi na mji wa Djibo katikati ya mwezi Mei, yamesababisha vifo vya wanajeshi 200.

Na nchini Niger, wanajeshi zaidi ya 100 waliuawa katika mashambulizi mawili eneo la Tahoua 24 Mei na eneo la Dosso 26 Mei, vyanzo vya usalama vilisema.

Nchi zote Burkina Faso na Niger hawajaweka wazi idadi kamili ya waliouawa.

CHANZO:TRT Afrika and agencies
Kionjo cha TRT Global. Tupe mrejesho wako.
Contact us