Takriban watu tisa waliuawa na wanne kujeruhiwa Jumapili katika shambulio la magaidi wa Boko Haram dhidi ya jamii ya Malam Fatori katika jimbo la Borno kaskazini mashariki mwa Nigeria.
Sugun Mai Mele, kamishna wa serikali za mitaa, alisema tukio hilo lilitokea karibu kilomita 270 (maili 167) kutoka mji mkuu wa jimbo la Maiduguri.
Pia aliongoza ujumbe kwa niaba ya Gavana Babagana Umara Zulum, ambaye kwa sasa yuko katika safari rasmi nje ya nchi, kuomboleza na familia za wahasiriwa.
"Tuko hapa kwa kumuakilisha Mheshimiwa, Gavana Babagana Umara Zulum, ambaye yuko nje ya nchi kwa kazi rasmi, kuwapa pole watu wa Malam Fatori kwa shambulio la hivi majuzi," ilisema taarifa.
Alihakikisha kuwa serikali ya jimbo la Borno na wanajeshi watafanya kila linalowezekana ili kulinda jamii.
"Malam Fatori ni eneo moja la serikali za mitaa ambalo tumedhamiria kuhakikisha uthabiti wake kwa sababu ya umuhimu wake wa kimkakati, na kuwataka watu kuwa wastahimilivu zaidi na wasali ili kuepusha matukio yajayo," ilisema taarifa hiyo.
Kamishna huyo aliongeza kuwa wachimbaji watatumwa kuchimba mitaro kuzunguka makao makuu ya serikali ya eneo hilo ili kuepusha mashambulizi yajayo ya waasi wa Boko Haram.
Pia aliwaonya wakazi dhidi ya aina yoyote ya ushirikiano na waasi, akisema yeyote atakayepatikana na hatia atakabiliwa na madhara.
Ili kusaidia kila familia ya wahasiriwa, naira 500,000 (dola 326) zilitolewa, huku waathiriwa wanne waliojeruhiwa wakipokea naira 250,000 (dola 163) kila mmoja.
Usman Tar, kamishna wa habari na usalama wa ndani, pia alitangaza mipango ya kuwapa makazi familia 3,000 waliokimbia makazi yao huko Malam Fatori, na kufanya jumla ya kaya zilizohamishwa kufikia 5,000.
"Acha niwahakikishie watu kwamba serikali ya jimbo iko tayari kutoa mipango muhimu ya usalama, kutoa rasilimali muhimu na usalama ili kuunganisha makazi yao katika nchi yao," alisema.
Hata hivyo kuibuka tena kwa mashambulio ya kundi la Boko Haram katika miezi ya hivi karibuni yametikisa eneo la kaskazini mashariki mwa Nigeria na kuzua hofu kuhusu kurudi kwa ukosefu wa usalama.