Nchini Kenya watu wasiopungua 10 wameuawa na wengine 29 kujeruhiwa wakati wa maandamano ya siku ya Saba Saba, Tume ya Kitaifa ya haki za Binadamu imesema Jumatatu.
Tume hiyo imebaini matukio mawili ya utekaji pamoja na watu 37 kukamatwa katika kaunti 17, ilisema katika taarifa.
Pia imesema kuwa kulikuwa na uporaji katika kaunti sita, na ofisi moja ya kuratibu masuala ya eneo bunge mkoa wa kati ilichomwa moto na wanaoshukiwa kuwa wahalifu.
Maandamano yaliyoongozwa na vijana
Waliouawa ilikuwa katika mitaa ya Kangemi mjini Nairobi na Kaunti ya Kajiado eneo la Kitengela, kulingana na vyombo vya habari vya nchini humo, vikinukuu wahudumu wa afya waliokuwepo kwenye eneo la tukio.
Maafisa wa uokoaji wanasema wamepata tabu kuwafikia waliouawa baadhi ya maeneo ya Kangemi kutokana na vizuizi vilivyowekwa na waandamanaji, kufanya iwe vigumu kwa magari ya kubeba wagonjwa kufikia sehemu hiyo.
Maandamano ya Saba Saba, yalikuwa kuadhimisha mapambano ya demokrasia nchini Kenya ya Julai 7, 1990, na maelfu ya watu walikuwepo barabarani.
Yakiwa yamechochewa na ugumu wa maisha, ukatili wa polisi, na msururu wa mauaji ya watu wakiwa chini ya ulinzi wa polisi, maandamano haya yaliratibiwa na vijana wa Kenya.
Silaha na mabomu ya machozi
Walioshuhudia tukio la Kangemi wanaeleza kuwepo kwa makabiliano kati ya maafisa wa usalama na waandamanaji, huku kukiwa na milio ya risasi asubuhi yote.
Eneo la Kitengela, wakazi wanasema polisi walitumia risasi za moto na mabomu ya machozi kuwatawanya waandamanaji waliokuwa wanarusha mawe.
Tume hiyo ya haki za binadamu inaonya kuwa huenda idadi ya waliouawa ikaongezeka, huku ikibainika kuwa wale waliojeruhiwa wamepelekwa hospitalini. Bado hali ni tete katika mitaa ya mijini, ikiwemo ile ya Nairobi kama Kibra, Mathare, na Githurai, ambapo waandamanaji waliwasha moto na kuweka vizuizi katika barabara kubwa kwa kuweka kifusi.
Maandamano ya Jumatatu ya Saba Saba yanatokea huku kukiwa na wito kote nchini wa kumtaka Rais William Ruto kujiuzulu, polisi kutakiwa kuwajibika, na mabadiliko ya kiuchumi.