Simba Sports Club ya Tanzania itakuwa na kibarua kigumu cha kupindua matokeo baada ya kupoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya Al Masry ya nchini Misri katika mchezo wa kwanza wa hatua ya mtoano ya Kombe la Shirikisho la CAF uliofanyika Misri, Aprili 2, 2025.
Mabao ya Al Masry yalifungwa na Abderrahim Deghmoum katika dakika ya 16 ya mchezo kabla ya John Okoye Ebuka kuhitimisha karamu ya magoli katika dakika ya 89, katika mchezo ambao kwa kiasi kikubwa, ulitawaliwa na ‘Wekundu wa Msimbazi.’
Katika mchezo huo, Simba ilikuwa na umiliki wa mpira wa asilimia 59 dhidi ya 41 kutoka kwa wapinzani wao.
Hata hivyo, Simba itapaswa kuilaumu safu yao ya ushambuliaji, ambayo ilionekana kuwa butu kwa sehemu kubwa ya mchezo huo.
Simba ilicheza pasi nyingi zaidi katika mchezo huo, ikiwa imecheza pasi 503 huku Al Masry wakiwa na pasi 347.
Kwa upande wa mashambulizi langoni mwa timu pinzani, Simba Sports Club ilipiga mashuti 18 dhidi ya 7 yaliyopigwa na wapinzani wao.
Swali kubwa vichwani mwa Watanzania na mashabiki wa wawakilishi hao wa pekee wa Tanzania katika michezo ya kimataifa, ni iwapo ‘Wekundu wa Msimbazi’ watakuwa na uwezo wa kulipiza kisasi dhidi ya Wamisri hao, wakati watakapokutana tena Aprili 9, 2025 kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.