Jeshi la Somalia limeua magaidi wapatao 47 wa kikundi cha al-Shabaab katika mashambulizi tofauti, likiwemo moja lililotokea katika jimbo la kati la Shabelle.
Katika taarifa yake, Wizara ya Habari ya Somalia, imesema kuwa katika shambulio moja la angani katika wilaya ya Adan Yabaal ilitekelezwa kupitia msaada wa Kamandi ya Afrika ya Jeshi la Marekani (AFRICOM).
“Ripoti za awali zinaonesha kuwa watu 12 wakiwemo viongozi wa kikundi hicho waliteketezwa,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Mashambulizi hayo yanakuja siku moja baada ya magaidi hao kuudhibiti mji Adan Yabaal, ulioko kilomita 245 kutoka mji mkuu wa Mogadishu.
Mji huo una umuhimu wa kijeshi ukitumika kama kiunganishi kati ya jimbo la Hirshabelle na Galmudug.
Jeshi la Somalia lilikomboa mji huo kutoka kwa magaidi wa al-Shabaab, wakati wa operesheni ya kijeshi ya mwaka 2022.
Katika hatua nyingine, wizara hiyo imetoa taarifa za mauaji ya magaidi 35 wa kikundi cha al-Shabaab baada ya vikosi vya Darwish kudhibiti na kuwashinda magaidi hao katika kambi ya jeshi iliyopo katika eneo la Baidoa, siku ya Alhamisi.