Wanajeshi kumi na mbili wa Uturuki wamekufa mashahidi baada ya kuingiwa na gesi ya methane wakati wa msako kaskazini mwa Iraq, Wizara ya Ulinzi ya Uturuki ilitangaza siku ya Jumatatu.
Tukio hilo lilitokea siku ya Jumapili wakati wa msako ndani ya jabali lenye urefu wa mita 852 kwenye eneo la operesheni ya Claw-Lock, ambapo magaidi wa kundi la PKK walikuwa wamejificha.
Operesheni hiyo ilikuwa sehemu ya juhudi za kuuchukua mwili wa mwanajeshi mmoja aliyekufa shahidi ambaye aliuawa na magaidi wa PKK 2022. Wakati wa operesheni hiyo, wanajeshi 19 waliathiriwa na gesi, na wanne wakafariki, kufanya idadi ya waliofariki kufikia 12.
Waziri wa Ulinzi wa Uturuki Yasar Guler amesafiri hadi katika eneo hilo pamoja na makamanda waandamizi wa jeshi kukagua eneo la tukio na kuhudhuria hafla ya kuwaaga wanajeshi waliofariki.
“Tungependa kutoa rambirambi zetu za dhati kwa familia za mashahidi wetu, Jeshi la Uturuki, na taifa letu tukufu,” wizara hiyo ilisema katika taarifa, na pia tunawatakia afuweni ya haraka wale waliojeruhiwa.
Kundi la PKK, ambalo limeorodheshwa kuwa la kigaidi na Uturuki, Marekani, na EU, limekuwa likijihusisha na uasi wa umwagikaji mkubwa wa damu dhidi ya taifa la Uturuki kwa zaidi ya miongo minne.
Ili kukabiliana na vitisho hivyo, Uturuki ilianzisha Operesheni Claw-Lock 2022, ikilenga maeneo ambayo PKK inajificha sehemu za Metina, Zap, na Avasin-Basyan kaskazini mwa Iraq.
Mara nyingi kundi hilo hutumia kambi za kaskazini mwa Iraq kupanga na kushambulia upande wa pili wa mpaka dhidi ya Uturuki.
Mamlaka za Uturukli zimekuwa zikisisitiza mara kwa mara kuwa hatua zake ni kulingana na kifungu cha 51 cha utaratibu wa Umoja wa Mataifa, ambacho kinawapa haki ya kujilinda inaposhambuliwa kwa silaha. Pamoja na hayo, makubaliano ya mataifa mawili kati ya Uturuki na Iraq yanaruhusu Uturuki kufanya operesheni dhidi ya magaidi katika ardhi yao.